Makala

Mwaka mwingine wa Boni Khalwale bintiye akikwangura B+

January 8th, 2024 2 min read

SAMMY WAWERU na FRIDAH OKACHI 

BINTIYE Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ni miongoni mwa watahiniwa waliofanya bora zaidi katika Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) 2023.

Saa chache baada ya Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu kutangaza rasmi matokeo hayo mnamo Januari 8, 2024, katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi, Mjini Eldoret, mwanasiasa huyo alichapisha kupitia mitandao ya kijamii matokeo bora ya mwanawe.

Alisherehekea bintiye kukwangura alama ya B+ kwenye akaunti yake rasmi ya X (awali Twitter) na Facebook.

Mwanawe alikuwa akisomea katika shule moja ya upili eneobunge la Kiminini, Trans Nzoia.

“Hongera, Gift Atubukha Khalwale! Ninataka kushukuru familia yangu, Shule ya Upili ya St Brigids-Kiminini, na zaidi ya yote, Mungu kwa kusaidia Tubu wangu kuzoa alama za kufurahisha,” aliandika Seneta huyo.

Dkt Khalwale, ambaye alifanikiwa kurejea tena katika ulingo wa kisiasa uchaguzi mkuu 2022 kupitia tikiti ya United Democratic Alliance (UDA), alifichua alama ambazo bintiye alipata.

Aidha, alizoa alama ya B kwenye Somo la Kiingereza, Kiswahili, na Bayolojia, kila somo, na B – katika Hisabati.

Fizikia ilipata C, Kemia B +, Historia na Masuala ya Uongozi wa Serikali A, na Elimu ya Dini ya Kikristo A -.

Seneta Khalwale alipakia picha ya mwanawe aliyeonekana kujawa na furaha, akiwa amevalia blauzi ya manjano na suruali ya samawati iliyochakaa.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo wa serikali tawala ya Kenya Kwanza kusherehekea mafanikio ya watoto wake katika KCSE.

Mwaka 2022, bintiye mwingine alifanya vizuri katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, ambapo alizoa A – ya pointi 75.

Hali kadhalika, ndugu pacha wa binti huyo alipata C + ya alama 47 mwaka huo huo.

Maarufu kama ‘Bull Fighter’, Dkt Khalwale pia alisherehekea mwanawe mwingine kwa kupata B + ya alama 67 KCSE 2021.

Kwa muda wa miaka kadhaa, mwanasiasa huyo kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya amekuwa akisherehekea matokeo ya watoto wake katika Mtihani wa Kitaifa Shule ya Msingi (KCPE).

Mitandaoni, Wakenya hawakosi kummiminia sifa chungu Dkt Khalwale wakimtaja kama “mzazi mwenye bidii za mchwa kukwea mlima”.