Habari

Mwaka waanza kwa mbwembwe lakini pia majonzi

January 1st, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA wengi walisahau hali ngumu ya maisha waliyopitia 2019 kuukaribisha mwaka mpya wa 2020 kwa mbwembwe za kila aina wakilipua fataki na kuomba Mungu awalinde na kuwapa afueni mwaka 2020.

Hata hivyo, kwa baadhi ya familia, mwaka ulianza kwa huzuni na kilio baada ya wapendwa wao kuangamia kwenye ajali za barabarani na mikasa mingine.

Watu 10 walifariki kwenye ajali zilizotokea maeneo tofauti nchini siku ya kwanza ya mwaka 2020.

Katika miji mikubwa nchini, Wakenya walifurika katika maeneo ya burudani na ibada kukaribisha mwaka mpya kwa furaha.

Viongozi wa kisiasa na kidini walitoa wito wa umoja, uwiano, kuvumiliana na amani mwaka huu wa kwanza katika mwongo wa pili wa karne ya 21.

Watoto 16 walizaliwa katika hospitali ya Pumwani jijini Nairobi ilipotimu saa sita Jumanne usiku.

Katika kaunti ya Nakuru, wakazi walikaribisha mwaka kwa kuhudhuria tamasha mbili katika uwanja wa ASK mjini Nakuru, mkutano wa ibada katika uwanja wa michezo wa Afraha na katika hoteli ya Rift Valley Sports club ambako walitumbuizwa na wasanii mbali mbali.

Hata hivyo, katika kijiji cha Kihoto, eneo la Kabazi kaunti ya Nakuru, mafuriko ya hivi majuzi yaliwakosesha wakazi raha ya mwaka mpya.

Wakazi hao walisema ingawa wanashukuru Mungu kwa kuwavukisha mwaka salama, hawana cha kujivunia kwa sababu mimea yao ilisombwa na mafuriko.

Katika eneo la Pwani, wakazi, wageni na watalii mbalimbali walikaribisha mwaka kwa mtindo wa aina yake, wakijivinjari ndani ya bahari na maeneo ya burudani.

Mashua zilizojaa wakazi na watalii zilionekana zikizunguka baharini huko Lamu na nyingine kusimama katikati ya bahari zikiwa zimepambwa kwa mataa ya rangi tofauti na kuleta mvuto wa aina yake.

Mamia ya wakazi walijumuika katika bustani ya Kibarani kualika mwaka mpya. Hafla hiyo iliandaliwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ambaye aliwahimiza wakazi kuishi kwa amani.

Katika kisa cha huzuni, watu watano walifariki Jumatano katika ajali iliyotokea kwenye barabara ya Eldama Ravine kwenda Eldoret, kaunti ya Baringo. Ilisemekana watu hao walikuwa wakitoka sherehe ya kukaribisha mwaka ajali ilipotokea.

 

Na BENSON MATHEKA, SAMUEL BAYA, VITALIS KIMUTAI, ERIC MATARA, KALUME KAZUNGU, na DIANA MUTHEU