Michezo

Mwalala pua na mdomo kurejelea majukumu yake ya ukocha

June 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Bandari FC, Bernard Mwalala amefichua kwamba yuko pua na mdomo kurejea katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) huku vikosi vitatu vya haiba kubwa vinavyoshiriki kipute hicho na vingine kutoka Tanzania na Rwanda vikiwania huduma zake.

Kocha huyo wa zamani wa Nzoia Sugar hajakuwa na klabu tangu asimamishwe kazi kisha kutimuliwa na Bandari FC mnamo Januari 2020 kutokana na msururu wa matokeo duni.

Hata hivyo, Mwalala ambaye ni miongoni mwa wakufunzi wachanga zaidi katika soka ya humu nchini, analenga kurejea kwa matao ya juu zaidi pindi kivumbi cha KPL kitakaporejelewa baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.

Mwalala ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Harambee Stars alirejea nyumbani kwao mjini Kitale tangu aagane rasmi na Bandari.

Ameshikilia kwamba kwa sasa anatathmini ofa zote ambazo amezipokea kutoka kwa klabu tatu zinazomvizia kabla ya kuamua pa kutua kwa minajili ya kampeni za muhula ujao.

Hata hivyo, Mwalala amekataa kufichua majina ya vikosi hivyo vinavyomhemea humu nchini na katika mataifa ya Rwanda na Tanzania.

“Nimekuwa katika mazungumzo na klabu tatu na nina hakika kwamba nitajiunga na mojawapo kabla ya msimu mpya wa 2020-21 kuanza,” akatanguliza Mwalala katika mahojiano na mojawapo ya magazeti ya humu nchini.

“Maisha nje ya uwanja ni mazuri japo napania sana kurejelea ukocha ambacho ni kitu najivunia kufanya. Nimetumia muda huu nje ya uwanja kuwazia kuhusu masuala mengi na malengo yangu binafsi ninayoazimia kuyaafikia katika ulingo wa ukufunzi,” akadokeza.

Mnamo Novemba 2019, Mwalala alikuwa akihusishwa pakubwa na miamba wa soka ya Tanzania, Yanga SC kabla ya kikosi hicho kujinyakulia huduma za mkufunzi wa zamani wa AFC Leopards, Luc Eymael mnamo Januari 2020.

Mwalala ambaye pia amewahi kuchezea Yanga katika enzi yake ya usogora, anaamini kwamba angalikuwa tayari amepata kikosi kipya cha kunoa isingalikuwa kwa janga la corona ambalo limevuruga mikakati ya vikosi kadhaa vilivyokuwa vikimkeshea.