Habari Mseto

Mwalimu abambwa baada ya kufumaniwa akinajisi mtahiniwa wa KCPE

October 15th, 2018 1 min read

Na VITALIS KIMUTAI

NAIBU mwalimu mkuu katika shule moja ya msingi Kaunti ya Bomet amekamatwa baada ya kupatikana akimnajisi mtoto wa darasa la nane.

Ilidaiwa mwalimu huyo alipatikana uchi akiwa na msichana huyo nyumbani kwa nyanyake ambako amekuwa akiishi. Nyanyake mwanafunzi huyo hakuwa nyumbani wakati wa kisa hicho.

Iliripotiwa kuwa mshukiwa aliingia nyumbani humo kimyakimya saa nne usiku lakini kile ambacho hakujua ni kwamba kulikuwa na mwanakijiji aliyemshuku ambaye aliita wenzake wakavamia boma hilo.

Wanakijiji walipofahamishwa kuhusu tabia za mwalimu huyo wa Shule ya Msingi ya Bukacha, walivunja mlango wa nyumba na walimkuta akimnajisi mwanafunzi huyo aliyepangiwa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka huu.

Katika hali hiyo, msichana alitorokea gizani lakini akakamatwa siku iliyofuata na kupelekwa kwa polisi ambao walimpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti iliyo Longisa ili afanyiwe uchunguzi wa kimatibabu.

“Mwalimu alikamatwa Ijumaa usiku akiwa na mkate na soda mbili ambazo inaaminika alitumia kumhadaa mwanafunzi huyo,” akasema chifu msaidizi anayesimamia lokesheni ndogo ya Bukacha, Bw Weldon Langat.

Bw Langat pamoja na wanachama wa kikundi cha Nyumba Kumi katika kijiji cha Bukacha, kaunti ndogo ya Bomet Mashariki walimwokoa mwalimu huyo ambaye nusura auawe na umati uliokuwa na hasira.

OCPD wa Bomet, Bw Samson Rukunga, alithibitisha kisa hicho na kusema mwalimu huyo atashtakiwa.