Habari

Mwalimu afa, watahiniwa 3 wajifungua KCSE ikianza

November 5th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MKASA ulikumba siku ya kwanza ya mtihani wa kitaifa wa shule za sekondari katika kaunti ya Nakuru baada ya mwalimu mmoja mkuu kufa katika ajali baada ya kuupokea mtihani wa shule yake.

Ajali hiyo iliyotokea mapema Jumatatu katika eneo la Longonot kwenye barabara ya Maai Mahiu-Naivasha, ilihusisha gari alilokuwemo mwalimu huyo na lori.

Kulingana na kamanda wa kaunti ndogo ya Naivasha Bw Samuel Waweru, gari hilo dogo lilipoteza mwelekeo na kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.

Walimu wengine wawili waliokuwa pamoja na marehemu walipatwa na majeraha mabaya na kisha kukimbizwa katika hospitali ya mishenari ya Kijabe.

“Mwalimu huyo mkuu aliaga dunia papo hapo huku wenzake wawili wakikimbizwa hospitalini kwa ili kupokea matibabu,” akasema Bw Waweru.

Watatu hao ni walimu wa shule za upili za Rev Jeremiah Gitau, Mustard Seed na Kiambogo.

Naibu kamishna wa Naivasha Mbogo Mathioya alisema mpango ulifanywa kwa haraka na kuhakikisha kuwa mitihani hiyo ingewafikia watahaniwa kwa wakati ufaao.

Mjini Nakuru, takribani watahiniwa watano waliufanya mtihani huo katika hospitali mbalimbali.

Mkurugenzi wa elimu Bw Lawrence Karuntimi alisema kwamba kati ya watano hao, wasichana watatu waliufanya mtihani wao katika wadi ya kujifungua huku wawili wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Nakuru Level Five.

Kule Molo, mtahiniwa wa kujitegemea katika shule ya upili ya Njega Karume alianza mtihani wake huku picha tofauti na yake ikiwa imebandikwa kwenye dawati lake.

Hata hivyo, mkurugenzi wa eneo hilo Vincent Rono alisema kuwa suala hilo lisingemzuia mtahiniwa huyo kuendelea na mtihani wake.

Mtihani ulianza kwa uzuni katika kaunti ya Migori baada ya mtahiniwa mmoja kufa maji siku moja kabla ya mtihani kung’oa nanga.

Tyson Suga mwenye umri wa miaka 19 alikuwa mwanafunzi katika shule ya upili ya Mtakatifu Paul Odendo.

Alisemekana kuwa alikuwa ameenda kuosha nguo zake katika eneo la Sori alipokumbana na maafa.

Kulingana na kamanda wa polisi wa Nyatike Bi Stella Too, marehemu aliondoka nyumbani kwao mnamo Jumapili jioni na kuelekea kwenye ziwa na baadaye mwili wake ukapatikana ukielea kwenye maji.

“Aliondoka kuenda kuufanya usafi kule kwenye ziwa lakini kwa bahati mbaya akafa maji. Ripoti kutoka kwa familia yake inaonyesha kuwa kijana huyo alikuwa na ugonjwa wa kifafa,” akasema BI Too.

Mwili wake umehifadhiwa katika kituo cha Sori Lakeside ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

Kule Kakamega, msichana aliyejaaliwa kupata pacha siku ya Jumapili, ni miongoni mwa watahiniwa wanaoendelea na mtihani huo.

Msichana huyo ni wa shule ya upili ya St Marys Ebusambe.

Mtahiniwa mwingine, Felix Nyongesa wa shule ya wavulana ya Koyonzo alifanyiwa upasuaji mnamo Ijumaa wiki iliyopita.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo alijaribu kuufanya mtihani wake shuleni lakini akalemewa na kusafirishwa hadi kwenye hospitali ya Koyonzo ambapo aliwekwa chini ya uangalizi wa madaktari.

Waziri wa elimu Prof George Magoha aliwaonya matapeli kuhusu wizi na kuwauzia wazazi mitihani hiyo ili kuendeleza malego yao binafsi kwenye mtihani huo wa kitaifa ulioanza hapo Jumatatu.

Ripoti za Macharia Mwangi, Samuel Baya, Ian Omondi, Shaban Makokha na Elizabeth Ojina