Habari Mseto

Mwalimu ajitia kitanzi na kuacha ujumbe kushauri wanaume

July 9th, 2018 1 min read

Na GRACE GITAU

Polisi wanachunguza kisa ambapo mwalimu wa shule ya upili Kaunti ya Kirinyaga alijitia kitanzi na kuacha ujumbe akishauri wanaume kutafuta ushauri nasaha wanapopata matatizo ya kisaikolojia.

Mwalimu huyo, Charles Karimi Muriithi mwenye umri wa miaka 49, ambaye alikuwa akifunza shule ya upili ya Thaita, alijitoa uhai kwa kujitia kitanzi ndani ya nyumba yake iliyoko kijiji cha Kirigo.

Alikuwa akiishi peke yake kwa sababu mkewe ni mwalimu katika shule moja Kaunti ya Nyeri.

Kulingana na Naibu wa chifu wa eneo hilo, Jamleck Kabui, marehemu alimuagiza kijana jirani kumtembelea baada ya dakika 30 lakini alipowasili katika nyumba yake alipata mwili wake ukining’inia kutoka paani. Kijana huyo alimwarifu chifu na maafisa wa polisi.

Kulikuwa na karatasi kwenye meza iliyokuwa na ujumbe alioandika. Alieleza aliyokuwa akipitia na uamuzi wake wa kujiua,” alisema afisa huyo wa utawala.

Majirani pia walisema alikuwa mchangamfu na hakuwa na ugomvi na yeyote.

Walishangaa aliamua kujitia kitanzi na kilichosababisha ajitoe uhai.

Hiki ni kisa cha pili cha mwalimu kujitia kitanzi katika kijiji hiki baada ya mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Kirigo kujiua mwaka wa 2015.