Habari Mseto

Mwalimu aliyeanguka ofisini na kufariki ghafla kuzikwa Ijumaa

February 8th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MWALIMU mkuu wa Shule ya Upili ya Mukuria iliyoko Kaunti ya Murang’a aliyeanguka ghafla na kuaga dunia mnamo Februari 2, 2024, akiwa ofisini mwake, atazikwa Ijumaa.

Bi Faith Njoki Kariuki alifika shuleni akionekana kuwa buheri wa afya lakini akaanguka ghafla ofisini mwake na kuaga dunia.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kandara Peter Maina, mwalimu huyo alianza kuhisi unyonge na ndipo akaingia ofisini mwake kutulia.

Aliongeza kwamba muda mfupi baadaye, walimu wengine walisikia kishindo katika ofisi ya mwalimu huyo na walipoingia kujua kiini, wakakumbana naye akiwa hoi sakafuni.

Bw Maina alisema kwamba harakati za kumpa huduma ya kwanza ziliingiwa na taharuki baada ya wenzake kugundua hakuwa akipumua.

“Alipelekwa upesi katika hospitali iliyo karibu na baada ya kutambulika kwamba tayari alikuwa ameaga dunia, mwili wake ukapelekwa hadi mochari ya Montezuma Monalisa iliyoko katika mtaa wa Kabati,” akasema.

Mumewe marehemu, Bw Daniel Kariuki Mundati ambaye ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya St Martin’s Maikuu iliyoko Kaunti ya Makueni, amesema kwamba mazishi yatakuwa katika kijiji cha Thakwa eneobunge la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Marehemu ameacha watoto wawili, wa kike na kiume, na alikuwa mzawa wa Kaunti ya Kirinyaga katika familia ya watoto tisa.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Elimu katika Bunge la Seneti, alisema kwamba amewasiliana na wadau katika shule hiyo na kuwasilisha risala zake za rambirambi.

Bw Nyutu alisema kwamba kwa sasa juhudi za kuandaa mikutano ya wadau zimeanza kuambwa ili mwalimu huyo apewe heshima zake za mwisho.

Waziri wa Ardhi Alice Wahome ambaye alihudumu kama mbunge wa Kandara kati ya 2013 na 2022 alitoa risala zake za rambirambi akimtaja mwendazake kama “mzalendo, mpole na mwenye kujituma kuhudumia sekta ya elimu eneo hilo”.

[email protected]