ZARAA: Mwalimu anayejituma ili kufufua kilimo cha kahawa

ZARAA: Mwalimu anayejituma ili kufufua kilimo cha kahawa

NA SAMMY WAWERU

MATHIRA ni mojawapo ya maeneo yanayochangia uzalishaji wa kahawa nchini.

Likiwa ndani ya Kaunti ya Nyeri, wengi wa wakulima walikuwa wameacha upanzi wa zao hilo kufuatia malipo duni.

Kabla ya Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta wakati akiwa mamlakani kuweka mikakati kuboresha sekta ya kahawa, baadhi hata walikuwa wameng’oa mikahawa, gharama ya juu ya uzalishaji ikiwalemea. Antony Mwema, mkazi na mkulima hakufa moyo na mageuzi yalipofanyika sasa anaridhia kahawa.

Akiwa mwalimu mstaafu wa Taasisi ya Kiufundi ya Mung’aria, Nyeri, aliingilia kilimo cha kahawa 2012. Alirithi shamba la wazazi wake, kufikia leo akiwa na idadi jumla ya mikahawa 300.

“Nilirithi idadi hiyo hiyo. Wazazi hawakuwa wakiitunza kwa sababu ya malipo duni,” asema, akidokeza kwamba ilimgharimu Sh30,000 kuifufua.

Mbali na kahawa, wakazi Mathira pia hulima mahindi, maharagwe, mseto wa matunda na wengine kufuga ng’ombe wa maziwa.

“Kuwepo kwa biashara mbadala za kilimo, wengi hawakutilia maanani kahawa kwa sababu ya malipo mabovu,” Mwema asimulia.

Miaka 10 baadaye, anasema hajutii uamuzi wake kusimama kidete na kahawa licha ya mahangaiko.

Chini ya mageuzi yaliyoanzishwa na Rais Kenyatta kupitia Wizara ya Kilimo, mkulima huyo anasifia malipo ya mwaka uliopita, 2021. Huuza mazao kupitia kiwanda cha Karie, ambacho ni mwanachama wa Rutuma Amalgamated Farmers’ Co-operative Society.

“Malipo ya 2021, kilo moja tulilipwa Sh109. Yalikuwa ya juu zaidi katika historia yangu kukuza kahawa,” afichua.

Miaka ya awali, Mwema anadokeza kwamba kilo moja ilikuwa ikichezea Sh50 – 70.

Kulingana na data za New KPCU, shirika la kiserikali linalojukumika kutafutia kahawa soko, 2021 kilo moja ilinunuliwa kati ya Sh85 – 128.

“Yalikuwa malipo ya juu zaidi wakulima kuwahi kupata Kenya,” asema Timothy Mirugi, Meneja Mkuu.

Shirika hilo aidha lilifanyiwa mabadiliko 2019, Mirugi akisema kuzinduliwa kwa kiwanda cha serikali kusaga kahawa na kuongeza thamani kulichochea ushindani mkuu sokoni.

Mabadiliko hayo vilevile yanajumuisha mikopo ya riba nafuu, mbolea inayosambazwa chini ya mpango wa ruzuku na kusaka mianya ya masoko yenye ushindani mkuu ndani na nje ya nchi.

Mwaka 2021, Mwema alivuna kilo 5,000 idadi hiyo ikiwa ya juu ikilinganishwa na kilo 1, 500 alizokuwa akivuna miaka ya awali. Hulima kahawa halisi ya Ruiru 11, akielezea kwamba anaendeleza kampeni kuhamasisha wakulima Nyeri kurejelea kilimo cha zao hilo maarufu kama dhahabu nyeusi.

Antony Mwema akielezea jinsi kahawa aina ya SL inapandikizwa na Ruiru 11. PICHA | SAMMY WAWERU

Wakulima wengi eneo hilo wangali mateka wa kahawa asilia aina ya SL, Mwema akijituma kuwasambazia matawi ya Ruiru 11 kupandikiza.

“Aina hii mpya ya kahawa inahimili mkumbo wa magonjwa na wadudu, mazao yake yakiwa mengi,” asema. Anadokeza kwamba kwa sasa anahudumu na zaidi ya wakulima 100.

“Sote tukikuza Ruiru 11, mazao yataimarika na mapato yawe bora jamii ipige hatua mbele kimaendeleo.”

Kwenye mahojiano ya kipekee shambani mwake, aliambia Akilimali kwamba mpango huo unanogesha Kiwanda cha Karie hivyo basi wanunuzi kumezea mate mazao yao. Mkulima huyo hata hivyo, alilalamikia bei ya juu ya pembejeo, akihimiza serikali kuitathmini zaidi.

“Dawa zingali ghali, hatua inayolemaza jitihada za wengi.”Amerika na Korea Kusini ndio wanunuzi wakuu wa kahawa ya Kenya.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto na Raila wakome kushikilia misimamo...

UFUGAJI: Ufugaji wa ndege aina ainati unavyompa kipato

T L