Habari Mseto

Mwalimu avamiwa na watu wasiojulikana

October 18th, 2020 1 min read

NA WAIKWA MAINA

Mwalimu wa shule ya msingi anauguza majeraha kwenye hospitali ya Kinangop baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana alipokuwa akienda kazini Alhamisi asubuhi.

Bi Emma Wanjiru, mwalimu wa Shule ya Msingi ya Roma Junior aliachwa na majeraha kichwani, shingoni na miguuni.

Bi Wanjiru alisema kwamba aliona mwanamume aliyekuwa amevalia koti lililokuwa limefunika kichwa  akimkimbiza na kuamua kumpisha.

Hapo ndipo mwanamume  huyo alimshika shigoni na kutoa kisu kutoka mfukoni na kumdunga mara kadhaa.

“Nilipiga duru na nikaanguka,” alisema Bi Wanjiru.

“Aliongeza kwamba nia yake ilikuwa ni kuniua. Sijui kwa nini. Sijui aliyenivamia ni nani kwani alikuwa amejifunika usoni.”

Mumewe mwalimu huyo Bw Maina Kimari alisema kwamba alishangazwa na tukio hilo na kwamba alikuwa anataka polisi wachunguze kisa hicho na kukamata wavamizi hao.

“Nilipigwa na butwaa kwani alitoka nyumbani kama kawaida kuelekea kazini . Nilipokea simu kutoka kwa watu walioitikia kilio chake ,” aliogeza.

“Nashukuru Mungu kwamba aliponea na kwamba anaendelea kupokea matibabu,” alisema Bw Kimari.

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA