Makala

MWALIMU KIELELEZO: Eunice Abuodha wa Kaunti ya Mombasa

November 4th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

SAWA na hali ilivyo katika mataifa mengi, shule za humu nchini pia hazina walimu wa kutosha waliotayarishwa na kuhamasika vizuri kwa minajili ya kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hali hii huathiri vibaya mafanikio ya kielimu ya watoto hawa na mara nyingi walimu hukosa mafunzo au msaada katika kuwafundisha watoto wa aina hii.

Viwango vya kitaifa kwa ajili ya mafunzo ya ualimu vinatofautiana kati ya nchi na nchi, na aghalabu mafunzo hayo huwa duni. Ni mara chache sana ambapo mafunzo ya ualimu kwa walimu wa kawaida hujenga hali ya kujiamini, maarifa na stadi mbalimbali za kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu na ambao wana mahitaji maalumu.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Eunice Abuodha ambaye kwa sasa ni mwalimu wa chekechea katika mojawapo ya shule maarufu jijini Mombasa.

Eunice anashikilia kwamba ipo haja kwa watunga-sera na wakufunzi wa walimu kuelewa vyema elimu jumuishi ili waweze kukuza kiwango cha kushirikishwa kwao katika masuala mbalimbali.

Eunice alizaliwa mnamo 1977 katika kijiji cha Kapuonja, Kaunti ya Kisumu. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto watatu wa marehemu Bw George Abuodha na Bi Fiprosa Abuodha. Nduguze Eunice ni marehemu Gordon Abuodha na Bi Rose Akinyi.

Eunice alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Sinyolo, Kisumu mnamo 1984. Huko ndiko alikosomea hadi mwishoni mwa 1991 alipofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE).

Alama nzuri alizojizolea katika mtihani huo zilimpa nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Bar-Union, Kisumu kati ya 1992 na 1995. Kati ya walimu waliompokeza malezi bora ya kiakademia ni Bw Ochieng wa Shule ya Msingi ya Sinyolo na Bw Gerald Okutto aliyemfundisha katika Shule ya Upili ya Bar-Union.

Baada ya ndoto za kusomea udaktari kuzimika ghafla, Eunice aliolewa na mumewe mpendwa Bw Duncan Ochieng katika eneo la Seme, Kisumu mnamo 1996. Kufikia sasa, wamejaliwa watoto wanne – Moline Cynthia, 24, Immaculate Wendy, 18, Ezekiel Denzel, 14, na Jasmine Tamisha, 5. Denzel atakuwa mtahiniwa wa KCPE mwaka huu katika Shule ya Msingi ta Sparki, Mombasa.

Kabla ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Modern Montessori, Mombasa alikosomea kati ya 2003 na 2005, Eunice alikuwa tayari akifundisha katika Shule ya Nyali West Academy, Mombasa. Aliajiriwa na shule hiyo iliyoko katika eneo la Mvita mnamo 2001.

Baada ya kuhitimu ualimu, alifundisha katika Shule ya Msingi ya Papyrus Academy, eneo la Kisauni, Mombasa kati ya 2005 na 2006 kabla ya kuhamia katika Shule ya Msingi ya Small and Smart Academy, Mvita, Mombasa. Alihudumu huko kati ya 2007 na Juni 2010.

Kabla ya kujiunga na shule anayoifundisha kwa sasa, Eunice aliwahi kuajiriwa na mzazi mmoja katika Shule ya Msingi ya Aga Khan Academy kumfundisha mtoto mwenye mahitaji maalumu.

Alimwelekeza mwanafunzi huyo kati ya Julai 2010 na Juni 2011 shuleni Aga Khan na akasalia naye hata baada ya mwanafunzi huyo kuhamishiwa katika Shule ya Kimataifa ya Coast Academy alikosomea kati ya 2011 na 2016.

Eunice anakiri kwamba kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum ni wito; si kazi ya kufundisha tu!

“Siri ya kuwa mwalimu bora hasa kwa wanafunzi wa sampuli hii ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji. Kusoma kwingi, kufanya utafiti wa kina kuwahusu na kuwauliza wajuao pia kutakujenga kitaaluma,” anasema.

Ili kufikia kiwango cha uelewa kinachohitajika miongoni mwa watunga-sera na wakufunzi wa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, utetezi na jitihada za uelimishaji zinapaswa kutiliwa mkazo.

Hii ina maana kwamba walimu wanahitaji kukumbatia elimu jumuishi katika siku ya kwanza ya mafunzo yao ya ualimu. Walimu waliopo kazini pia wanahitajika kushiriki programu za kuwakuza kitaaluma.

“Mafunzo ya ualimu lazima yawe na uwiano wa nadharia na vitendo. Yanahitaji kuwa na uwiano wa kujifunza kuhusu dhana ya elimu jumuishi. Walimu wanapaswa kuangalia na kutekeleza nadharia hizi kivitendo huku wakisaidiwa na wenzao wenye uzoefu zaidi,” anasema Eunice kwa kusisitiza kuwa mafunzo yenyewe yanahitaji kuendana na mazingira na tamaduni za watu mbalimbali.

Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi za Eunice katika kuchangia maendeleo ya jamii tangu Julai 2020. Wakfu huo umemnufaisha Eunice kidijitali na kumpa jukwaa la kutalii mbinu tofauti za kufundisha wanafunzi wakati huu wa janga la korona.