Makala

MWALIMU KIELELEZO: Millicent Achieng wa Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe

December 16th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUJIFUNZA kusoma na kuandika ni kazi ngumu! Kwa sababu unataka wanafunzi wamakinikie masomo haya, ni muhimu ufanye darasa lako – na shughuli ambazo zinahamasisha ujifunzaji wa kusoma na kuandika – liwe la kusisimua kadri iwezekanavyo.

Wanafunzi wanahitaji kujua jinsi ya kuhusisha sauti na herufi, herufi na maneno, maneno na sentensi.

Michezo, michoro, picha za rangi, nyimbo na mashairi ambayo wanafunzi wanayajua vizuri – na ambayo wanaweza kuyaimba na kuyaghani kirahisi kwa kuonyesha vitendo –yanawasaidia kujenga mahusiano haya.

Njia nyingine ya kukuza uhusiano huo miongoni mwa wanafunzi wa madarasa ya chini ni kuwashirikisha katika usomaji na usimulizi wa hadithi.

Haya ni baadhi ya majukumu ambayo Bi Millicent Loice Achieng hujitahidi kufanya katika Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe, Kaunti ya Mombasa.

Bi Achieng anavutiwa sana na ualimu kiasi kwamba hata katika kipindi hiki cha janga la korona, amekuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi wa chekechea katika eneo la Mtongwe, Likoni anakoishi.

“Unaposoma na watoto, usiwafafanulie kila kitu kwenye picha za vitabu au michoro ya chati. Waulize wanafikiri kitu gani kitakachotokea au kitafuata baadaye. Kumbuka kuwapa fursa nyingi ili wazungumzie kuhusu unachowafundisha –wahusika katika hadithi, kilichotokea, wanavyojisikia kuhusiana na hadithi n.k.”

Bi Achieng amegundua kuwa wanafunzi wanahitaji mazoezi mengi ili wajiamini katika usomaji. Yeye hutengeneza nakala nyingi za machapisho ya michoro, picha na chati za herufi za alfabeti na nambari kwa minajili ya ufundishaji.

Aidha, hutunga mashairi mepesi na nyimbo ambazo wanafunzi wanazijua vizuri na nyingine ambazo ni mahsusi kwa ajili ya ufundishaji wa dhana mpya.

Wanafunzi huzitamka au huziimba kwa kuonyesha vitendo kuhusiana na tungo hizo wanapocheza.

“La muhimu zaidi ni kuwaambia wanafunzi wenyewe waguse, wasome herufi na maneno husika na kuyaonyesha ubaoni au kwenye chati huku ukiwasaidia kila wanapotatizika,” anasema.

Ikilazimu, Bi Achieng huandaa kadi zenye picha, nambari, herufi na maneno katika masomo saba anayoyashughulikia ili kuzitumia kwa njia nyingine na wanafunzi wake, ama kwa mmojammoja au katika vikundi vidogovidogo.

Bi Achieng anafarijika kuona kuwa mazoezi ya sampuli hii yanasaidia mno katika kuwafanya wanafunzi wajiamini na kusonga mbele.

“Kusoma na kuandika kunaweza kusisimua na kuchangamsha sana, lakini baadhi ya wanafunzi wanajenga mitazamo hasi kuhusiana na shughuli hizi,” anaeleza.

“Sababu inaweza kuwa ni kwa vile wanavyogundua kuwa kusoma na kuandika ni kugumu, labda kwa kuwa wanaweza kuchoshwa na kazi za usomaji na uandishi ambazo zinafuata ruwaza zilezile daima, au pengine hawaoni thamani kuu katika usomaji na uandishi.”

Mojawapo ya majukumu ya mwalimu ni kuamsha ari ya wanafunzi katika usomaji na uandishi na kuwafanya wahamasike zaidi.

“Hakuna kinachonipa fahari zaidi katika taaluma ya ualimu kuliko kutangamana na watoto wachangamfu kupitia michezo, uimbaji na utambaji wa hadithi. Watoto wanaweza hata kukufanya usahau shida na changamoto za maisha,” anakiri Bi Achieng.

Kwa mtazamo wake, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo wa kiwango cha chekechea ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na wanasahau haraka hata unapowaadhibu kwa utundu.

“Kudumisha urafiki na watoto humfanya mwalimu kuwa mkamilifu. Kilele cha urafiki huo ni pale wanafunzi wanapokukimbilia na kukupa hadithi za kila sampuli kuhusu maisha yao binafsi.”

Bi Achieng alizaliwa katika eneo la Changamwe, Mombasa na kulelewa katika sehemu za Majengo na Kongowea jijini Mombasa na eneo la Nyahera, Kaunti ya Kisumu. Wazazi wake ni Bw Robert Ayieko Othano na marehemu Bi Helidah Were.

Alianza safari yake ya elimu mwishoni mwa miaka ya 1970 katika chekechea ya Majengo Social Hall, Mombasa kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Achego, eneo la Songhor, Muhoroni.

Alifanyia mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya Khadija, Mombasa mnamo 1988.

Alifaulu vyema na kupata nafasi ya kusomea katika shule maarufu ya Matuga Girls, Kaunti ya Kwale kati ya 1989 na 1992.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), Bi Achieng alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Curtis Kongowea Baptist, Mombasa kati ya 1993 na 1996. Aliolewa mwishoni mwa 1996 na kuanza kufanya biashara katika eneo la Mtongwe, Mombasa.

Ilikuwa hadi 2006 ambapo alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John’s Kilimambogo, Thika. Alifuzu mnamo 2008 na akafundisha katika Shule ya Msingi ya Mtongwe kwa muda mfupi kabla ya kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe akiwa mwalimu wa kujitolea.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Bi Achieng kwa kandarasi mnamo 2010 kabla ya kumpa kazi ya kudumu mwaka mmoja baadaye na kumdumisha katika shule hiyo hiyo ya Kenya Navy Mtongwe.

Wakfu wa Aga Khan umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi zake za kuchangia maendeleo ya jamii na kuhakikisha kwamba anawapa wanafunzi malezi bora ya kiakademia katika eneo zima la Mtongwe tangu Julai 2020.

“Nilianza kuvutiwa na ualimu tangu nikiwa mtoto mdogo. Walimu walikuwa watu wa kuheshimika zaidi katika jamii. Walikuwa wamepiga hatua kubwa kimaendeleo na walitegemewa sana kwa ushauri wa kila aina. Ualimu ilikuwa kazi ya hadhi na ilikuwa tija kujihusisha nayo.”

Kati ya watu waliomhimiza sana Bi Achieng kujitosa katika taaluma ya ualimu ni mjomba wake, Bw Juma, aliyemfundisha katika Shule ya Msingi ya Achego.

Mbali na kufundisha wanafunzi wa chekechea hadi gredi ya tatu katika Shule ya Msingi ya Kenya Navy Mtongwe, Bi Achieng pia ni mwanakwaya stadi katika Kanisa la ACK St John’s Mtongwe. Uimbaji, ukulima na ufugaji ni kazi anazopania kumakinikia zaidi baada ya kustaafu.

Bi Achieng amejaliwa watoto wanne: Handel Offiro Juma, 23, Mozart Eshiteti, 22, Jester Ayieko, 15, na Christine Helidah Were, 9.