Habari Mseto

Mwalimu mwanablogu Kisii alinyongwa – Upasuaji

April 9th, 2024 3 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MWALIMU mwanablogu wa Kisii Duke Nyabaro, 31, ambaye mwili wake ulipatikana ukining’inia nje ya kibanda saa chache baada ya kutumia mtandao wa Facebook Jumapili, Aprili 7, 2024 alifariki kwa kunyongwa kwa mikono, mmoja wa maafisa wanaochunguza kisa hicho amefichua. 

Kachero huyo, aliyeomba tubane jina lake, kutokana na unyeti wa suala hilo aliambia Taifa Dijitali kwamba uchunguzi wa maiti uliofanywa kwa mwili wa marehemu Jumatatu asubuhi, Aprili 8, 2024 katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kisii (KTRH) uliashiria aliuawa.

“Koo lake lilionekana kufinywa ili asiweze kupumua. Uchunguzi wa kisa hiki umeshika kasi, tunafuatilia mawimbi ya mawasiliano ya simu yake ili kujua ni watu gani aliozungumza nao mara ya mwisho,” afisa huyo alisema.

Kabla ya kifo chake katika kijiji cha Nyaora Corner, eneobunge la Kitutu Chache Kusini, Bw Nyabaro ambaye pia alikuwa mwalimu wa shule ya upili, anasemekana kuonekana akiwa pamoja na baadhi ya marafiki zake katika maeneo maarufu ya burudani ndani ya mji wa Kisii.

Aidha, marafiki wawili ambao alikuwa nao walikuwa wanawake.

Duru zinaarifu walijivinjari hadi saa tatu usiku wa siku ya Jumamosi.

Bw Nyabaro amekuwa mtumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii ambaye mara nyingi alitoa maoni yake kuhusu siasa za Kisii, na hasa zile za eneobunge la Bonchari, ambako anatoka.

Wakati hakuwa akitoa maoni yake kwenye majukwaa yake, angekuwa darasani akifundisha katika Shule ya Upili ya Chacha Moronge iliyoko Kehancha, Kaunti ya Migori.

Mwili wake ulipogunduliwa, ulikuwa umefungwa mkanda shingoni.

Magoti yake yaligusa ardhi.

Wauaji wake walifanya hivyo ili kuwadanganya watu kwamba alikuwa amejinyonga.

Mbunge wa Bonchari Dkt Charles Onchoke, ambaye alitembelea makao makuu ya polisi ya Kaunti Ndogo ya Kitutu ya Kati Jumatatu asubuhi, alitoa wito wa uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo.

“Nimefurahishwa na maafisa wanaochunguza suala hili. Nimefanya nao mazungumzo na wamenieleza kuwa wamewahoji baadhi ya marafiki wa marehemu Nyabaro. Pia, wanatafuta wengine. Isitoshe, nimefahamishwa kuwa wauaji walitoroka na simu yake wakiwa kwenye pikipiki,” Dkt Onchoke alisema.

Akimmiminia sifa, mbunge huyo alimtaja marehemu kama mtu mwema aliyependa kazi yake.

“Tumesikitishwa na kifo chake. Nyabaro alikuwa kijana aliyependa kazi yake na kama jamii, tulikuwa na matumaini mengi kwake. Alikuwa mtu ambaye angesaidia jamii siku zijazo. Nikiwa mbunge wa Bonchari, nimempoteza rafiki yangu aliyekuwa akinisaidia katika baadhi ya kazi zangu. Tunataka kuwaambia wachunguzi waende kwa kasi na kutia nguvuni waliohusika kumpokonya uhai. Hatutakubali visa kama hivyo vya watu kuua wengine,” Dkt Onchoke aliongeza.

Joshua Masire, mjomba wa Nyabaro alisema marehemu alifiwa na mamake miaka mingi iliyopita alipokuwa na umri mdogo lakini walimlea inavyostahilio.

“Tulimlea vizuri. Tulihakikisha tunampeleka shule hadi alipomaliza chuo kikuu. Tulihakikisha anapata ajira. Alianza kufundisha kwa mara ya kwanza katika shule ya upili ya Nyambaria na baadaye akatumwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) huko Migori. Alikuwa mtu mzuri,” Bw Masire alisema.

Alimtaja mpwa wake kama mtu mzuri ambaye alikuwa mchangamfu na alijuta kwamba alipoteza maisha kwa namna hiyo, wakati walikuwa wameweka matarajio mengi kwake.

“Unapomsomesha mtoto, unatarajia mengi kwake na ni hasara alikumbana na kifo chake kwa njia kama hiyo. Aliuawa na hilo ndilo linalotuhuzunisha. Aliyeondoa uhai wa Nyabaro, tunakuombea usiwe na amani kamwe. Mungu atakuadhibu,” Bw Masire aliyehuzunika alilaani.

Mjombake huyo pia alifichua kuwa walikuwa na ugumu wa kupata mpasuaji wa kufanya uchunguzi wa maiti kwa sababu ya mgomo unaoendelea wa madaktari.

Lakini walifanya mipango ya kibinafsi na kumpata mpasuaji.

“Matokeo ya uchunguzi wa maiti yalifichua kuwa alinyongwa,” Bw Masire alisema.

Waumini wa kanisa waliogundua mwili wa Nyabaro walielezea jinsi nguo za marehemu hazikuwa zimelowa maji licha ya mvua kunyesha usiku kucha siku ya mkasa.

“Tunashuku mchezo mchafu. Kijana huyo hakujinyonga. Mvua ilinyesha usiku kucha na kuna unyevuunyevu kila mahali. Imekuwaje nguo zake zikabaki kavu nje ya kibanda alichopatikana?” Bw James Metobo, mkazi wa Nyaora Corner aliuliza.

Marehemu ameacha mke na watoto wawili, wa kiume na wa kike.