Makala

Mwalimu mwenye mikono ya dhahabu

August 21st, 2020 3 min read

Na Steve Mokaya

Tangu kuzuka kwa gonjwa la COVID-19, maelfu ya watu humu nchini na hata kwingineko wamepoteza ajira zao.

Wengi wanabambanya kuishi, na kudura ya Mwenyezi Mungu imewahifadhi hadi sasa, maadam kwa njia moja au nyingine, mikono iliyokuwa ikiwalisha ilikatwa na makali ya virusi vya Corona.

Hata hivyo, hali si sawa kwa kila mtu. Yaani, wapo wengine wachache, ambao kwao, satua iliyoletwa na COVID-19 ni baraka. Mmoja wao ni Delphine Moraa.

Moraa ni mwalimu aliyeajiriwa na serikali katika shule ya upili ya Eronge DEB katika eneo la Nyamira Kaskazini. Mbali na taaluma yake ya ualimu, amekuwa akitengeneza mikeka, nguo na viatu, japo kwa umakinifu mkubwa.

Umakinifu ambao umemwezesha kupata muda wa familia yake, wanafunzi wake shuleni na kufanya kazi yake ya kando, ukipenda side hustle. Ila sasa ako na wakati mwafaka na wa kutosha kufanya kazi hii kikamilifu. Lakini je, mwalimu huyu alipataje ujuzi huu? Anaeleza.

“Wajua chuoni kuna muda mwingi ambao mtu akitaka, anaweza kuutumia ukamfaidi. Nilipokuwa katika chuo kikuu cha Kenyatta, nilikuwa najipanga vizuri. Naamka asubuhi nafanya shughuli zangu kisha naelekea darasani.

Na nilikuwa nimefanya urafiki na mama mmoja aliyekuwa akishona nguo hapo karibu. Baada ya masomo ya siku, ningeenda kwake namnunulia chamcha kisha yeye ananipa mafunzo ya kushona nguo,” anasema.

Isitoshe, mbali na kupata mafunzo ya ushonaji, Bi Moraa alikuwa anajikidhia mahitaji yake chuoni kwa kuwasonga wanafunzi wenzake.

“Baada ya kumaliza kidato cha nne, niliambia mama akanipeleka kupata mafunzo ya ususi. Kwa hivyo, nilipokuwa najiunga na chuo kikuu, tayari nilikuwa na huo ujuzi.

“Sasa pale chuoni nikawa nawasuka wasichana wenzangu, hasa nyakati za usiku na pia wikendi. Hela nilizozipata zilinipiga jeki sana, kwani hata nilikataza wazazi kunitumia pesa za matumizi,” anasema.

Bi Moraa anasema kuwa baada ya kumaliza masomo yake ya chuoni, alikuwa amepata ujuzi wa kutosha na akawa tayari kuanza biashara ya kushona nguo.

“Nilipoajiriwa, kitu cha kwanza nilichonunua ni cherehani. Nikawa naitumia kufanya biashara hii,” anasema.

Anaongeza kuwa alianza kwa kuwashonea jamaa yake nguo, na ambazo zilimsaidia kutangaza bisahara yake.

“Nilishonea watoto wangu, bwanangu na hata mimi mwenyewe. Sasa nikiwa huko nje watu wangetamani kushonewa nguo kama hizo tulizovaa, na kuniomba niwaelekeze kwa fundi aliyezishona. Na hivyo ndivyo nilianza kupata wateja,” anasema.

Hata hivyo, Bi Moraa anasema kuwa mwanzoni haikuwa rahisi kwa watu kuamini kuwa yeye ni fundi wa nguo, na kuwa wateja wengine walikuwa wanadhani ni mzaa tu.

“Hata kuna mama mmoja alikuwa akieneza habari potovu kuwa ‘Yule mama hashoni nguo; anapelekea fundi mwingine anamshonea.’ Lakini kadri muda uliiposonga, watu walianza kuamini kuwa mimi ni fundi. Hata wengine huja nawashonea wakiwa hapa,” anasema.

Mbali na kushona nguo, Bi Moraa pia anatengeneza mikeka na hata viatu. Ila sasa ujuzi huo aliupata kwa kujifunza yeye mwenyewe.

“Nilitumia simu kujifunza. Nilienda tu kwa Google na kutafuta video za kutengeneza hivyo bidhaa. Nikaangalia nikijaribu kutengeneza, na baada ya muda nikawa nimejua,” anasema.

Anasema kuwa ufanisi wake hadi sasa umechangiwa pakubwa na ushirikiano mwema wa familia yake, na hasa bwanake.

“Hapendi kunisumbua. Kabla aniombe kumsaidia kitu, kwanza anauliza kama niko na wakati. Iwapo ninafanya kazi, ananiacha tu niendelee na kazi yangu. Wakati mwingine akija jioni kutoka kazini halafu apate ninashona na bado sijaandaa chajio, anaingia jikoni na anapika chakula. Wakati mwingine nikikosa mtaji ananipa hela ama ananinulia nyuzi na vitambaa vya ushonaji,” anasema.

Anasema kuwa kazi hii imemfanya apange muda wake vizuri hata zaidi, kuliko vile ingekuwa asingekuwa nayo.

“Shuleni ninakofunza, vipindi vyangu huisha saa kumi jioni. Baada ya hapo, nawaona wanafunzi walio na maswali kwa nusu saa. Ifikapo saa kumi ushei ninapanda pikipiki na kukimbia moja kwa moja hadi kwangu.

Nifikapo nyumbani ninaandaa chajio kisha nakaa kwenye mashine na kuanza kazi hadi saa tatu usiku. Fauka ya hayo, wikendi zangu, hasa Jumapili ninafanya kazi hii tu,” anasema.

Bi Moraa anasema kuwa hata mtoto wake mkubwa, ambaye yuko katika darasa la nane ameanza kujua kazi hii, na kuwa hilo linampa furaha.

“Si vizuri ufunze mtoto kushika kitabu peke yake. Mtoto hata hajui kupika, hajui hata kushona nguo ikiraruka, hajui kitu kingine…. maisha yajayo yatakuwa magumu sana iwapo mtu hana ujuzi mwingine, mbali na masomo ya darasani. Kwa sababu saa hii tunapoongea wapo watu waliohitmu na hawana kazi; na bado wengine wanasoma,” anasema.

Kwa vile yeye ni mwalimu, muda wake mwingi anakuwa na wanafunzi na anapenda kuwashauri. Hata wakati mwingine hupitisha ujuzi wake kwa wale wanaonyesha nia na moyo wa kutaka kujua. Dianah Nyaboke ni mmoja wao.

“Nilkuwa natafuta fundi wa kushona nguo, kitenge. Nikaelekezwa kwake. Akanishonea hiyo nguo na ikapendeza sana. Kutoka hapo nikawa na mshawasha wa kujua pia. Nikapata kuwa likuwa anashona mikeka, nikamwomba anionyeshe. Akanionyesha na nikajua,” Nyaboke anasema.

Hata hivyo anasema kuwa vijana wengi wana tatizo moja; kiburi.

“ Vijana wengi hujiweka katika daraja la maisha ambalo katika uhalisia hawajalifikia. Wengi wamekosa unyenyekevu. Wanatamani maisha ya mtu anayefanya kazi ya ofisini, lakini hawataki kujua alipitia wapi ndio afikie hapo. Wacha tuwe tayari kufanya kazi yoyote nafasi ijapo,” anasema.

Mbali na vijana, Bi Moraa pia anawashauri wale walioajiriwa kufanya jitihada kupata ujuzi mwingine.

“Kwa wale ambao tumeajiriwa, tusikae tu eti sasa sisi tuko na kazi. Kazi ya pili ni nzuri kila wakati. Chochote hutendeka. Hebu fikiria umepoteza kazi, utaendea nani eti sasa nilishe? anaongeza.

Bi Moraa anapanga kupanua biashara yake iwe kubwa na awe mshonaji tajika wa nguo katika eneo zima la Sironga na hata Nyamira. Kadhalika, anapanga kuanzisha shule ya kuwapa vijana mafunzo ya ufundi huu, mumo humo kwenye biashara hiyo, katika eneo lilo hilo la Sironga.