Mwalimu taabani kwa kumdhulumu mtahiniwa wa KCSE

Mwalimu taabani kwa kumdhulumu mtahiniwa wa KCSE

PIUS MAUNDU Na SAMMY WAWERU

MWALIMU mkuu wa shule moja ya upili Kaunti Ndogo ya Yatta, Kaunti ya Machakosi ameshtakiwa kwa madai ya kumdhulumu mtahiniwa wa kidato cha nne kisha kumfukuza shuleni, siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kitaifa, KCSE.

Kwenye stakabadhi za kesi iliyowasilishwa katika korti ya Kithimani, mwanafunzi huyo kupitia mlezi wake anadai alidhulumiwa na naibu mwalimu mkuu na mwalimu mwingine kabla kufurushwa shuleni.

Ripoti ya matibabu iliyowasilishwa kortini inaeleza mwanafunzi huyo wa Shule ya Upili ya Kyasioni, Kaunti Ndogo ya Yatta anauguza majeraha ya sikio kwa kuzabwa kofi mara kadhaa na Bw Daniel Muoki, mwalimu, akisaidiwa na naibu mwalimu mkuu Bi Lilian Maithya.

“Sikio la kushoto limeibuka na tatizo la kutoskia baada ya kudhulumiwa na mwalimu,” inaeleza ripoti hiyo, ikiongeza kwamba mtahiniwa huyo anapaswa kuhudhuria kliniki hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kulingana na stakabadhi za korti, walimu hao “walisababisha majeraha ya mwili kwa mtoto na kumtimua shuleni bila sababu zenye msingi wowote”.

Kwenye kesi hiyo pia, ambapo mlezi wa mwanafunzi huyo ameshtaki mwalimu mkuu, Bi Virginia Gitonga, imefichuka mtahiniwa huyo wa KCSE mwaka huu alifukuzwa shuleni kwa kuvalia “nguo za nyumbani” Machi 13, 2021.

Kwa mujibu wa stakabadhi za korti, mwalimu mkuu amejitetea akidai mwanafunzi huyo “alitoka shuleni kwa hiari na hakutaka kurejea tena”.

Hata hivyo, stakabadhi za korti zinaeleza mwanafunzi huyo hakutoka shuleni na badala yale alisalia kwenye lango la shule hadi saa kumi na mbili za jioni, akirai kuruhusiwa kurejea kwa sababu hakuwa na idhini ya kutoka au nakala inayoonyesha alitakiwa kuondoka.

“Baada ya walimu kumkataza kurejea, aliomba mpitanjia simu akaniarifu mahangaiko aliyopitia,” inaeleza ripoti ya mlezi wake.

“Nilichukua hatua nikapigia mwalimu mkuu simu, akaniambia mtoto alitoka shuleni kwa hiari na hakutaka kurudi tena. Hata hivyo, nilipomweleza yuko kwenye lango la shule akakatiza mawasiliano,” ripoti hiyo inafafanua.

Aidha, mwanafunzi huyo aliporejeshwa shuleni, Bi Maithya alikataa kumruhusu aingie.

Kulingana na wakili wa mtahiniwa, Japheth Juma wa kampuni ya Auka Edwin & Associates: “Mwanafunzi huyo ni mtahiniwa wa kidato cha nne, na anapaswa kuanza kufanya mtihani wa kitaifa Machi 26, 2021 na amenyimwa fursa kujiandaa kufanya mtihani wa mwisho ambao ni wa manufaa sana maishani mwake”, mbali na majeraha aliyopata na kufurushwa shuleni bila barua.

Pia, imebainika mwanafunzi huyo amekatazwa kuchukua vitabu vyake vya mazoezi, kusoma kujiandaa kwa minajili ya mtihani na vifaa vya binafsi vya matumizi, vyote vikiwa shuleni.

Dhuluma ya mwanafunzi huyo iliripotiwa katika makao makuu ya idara ya polisi, Yatta, huku uchunguzi ukitarajiwa kuanza juma hili.

You can share this post!

Mtangazaji wa zamani wa NTV afariki kutokana na corona

SAMIA SULUHU: Rais mtarajiwa wa Tanzania