Michezo

Mwalimu wa St Peters Mumias kuwania kiti cha FKF

May 21st, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MWALIMU Mkuu wa shule ya St Peters Mumias kutoka Kaunti ya Kakamega, Cosmas Nabongolo amejibwaga uwanjani kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi ujao wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

Nabongolo amefanya uamuzi huo siku chache tu baada ya aliyekuwa Katibu wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye kutangaza kuwania kiti hicho.

“Watu wameona mengi tuliyofanya mashinani na sasa wanatusukuma tupigania uongozi. Binafsi nimepata shinikizo kutoka kwa wadau wa soka nchini wanaonisihi nipiganie wadhifa huu. Niko tayari kushindana na iwapo nitapewa nafasi nitawatumikia Wakenya ipasavyo,” alisema Nabongolo ambaye anafahamika kwa kusaidia shule kadhaa zikiwemo Kapenguria, St Anthony Kitale kupata ufanisi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

“Nimejitokeza kwa sababu mchezo huu unaangamia chini ya uongozi wa sasa wa Nick Mwendwa. Tunataka kuwarejeshea matumaini vijana wetu, na wengine watakaozaliwa baadaye,” aliongeza Nabongolo.

Lakini uamuzi wake umepingwa na watu kadhaa, akiwemo kocha wa sasa wa Bishop Njenga Girls, Fred Serenge alimshauri asubiri hadi wakati mwingine.

Serenge alisema huenda Nabongolo akaendelea na mipango yake bila kuelewa jinsi kura za soka nchini zinavypigwa na baadaye kujuta.

Mbali na Musonye na Mwendwa, wengine waliotangaza kuwania kiti hicho ni aliyekuwa mwqenyekiti wa FKF, Sam Nyamweya, Afisa Mkuu wa Gor Mahia, Lodvick Aduda na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa FKF, Twaha Mbarak.