MWALIMU WA WIKI: Bi Wambui ni mwalimu kwa wito

MWALIMU WA WIKI: Bi Wambui ni mwalimu kwa wito

Na CHRIS ADUNGO

TIJA na fahari ya mwalimu yeyote aliye na wito wa kufundisha ni kuona mtoto aliyeingia shuleni bila kujua lolote akipiga hatua kubwa kielimu na kuanza kufahamu stadi za kusoma na kuandika chini ya uelekezi wake.

Kufundisha wanafunzi wa madarasa ya chini kunahitaji mwalimu kutumia mbinu mbalimbali zitakazompa majukwaa mazuri ya kushirikiana na watoto kutalii mazingira anuwai yatakayokuza viwango vyao vya ubunifu na kuwaamshia ari ya kuthamini utangamano.

Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua sana wanafunzi wa umri mdogo na kuchochea bongo zao kufanya kazi; matumizi ya nyimbo, video, vibonzo, michezo ya kuigiza, michoro na picha za rangi ni namna nyingine ya kufanya shughuli za ndani na nje ya darasa kuwa za kuvutia.

“Kuhusisha wanafunzi moja kwa moja katika usomaji, uimbaji, uchezaji au utambaji wa hadithi huchangia kujiamini kwao hata wasipokuwa vikundini. Mawanda ya fikira zao hupanuka upesi na huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno,” anasema Bi Joyce Wambui Mwangi.

Kwa mujibu wa mwalimu huyu wa shule ya msingi ya Gilgil Victory Academy (GVA), mbinu rahisi zaidi ya kuchochea wanafunzi kupenda masomo ni kuwaaminisha kwamba hakuna lisilowekezana.

“Kwa kuwa uwezo wa watoto wa kumudu masomo hutofautiana, mwalimu ana ulazima wa kuelewa kiwango cha kila mwanafunzi na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazowezesha wote kufikia malengo yao.”

“Shughuli za ujifunzaji na ufundishaji zitakuwa rahisi iwapo mwalimu atasikiliza wanafunzi, kuelewa changamoto zinazowakibili na kuwaelekeza ipasavyo hatua kwa hatua.”

“Atambue na kupalilia vipaji vya wanafunzi wake huku akiwatia moyo wale wanaotatizika kuelewa somo lake. Uhusiano wa karibu kati ya mzazi na mwalimu utafunua mengi kuhusu uwezo wa mwanafunzi katika nyanja mbalimbali. Ukishajua chanzo, suluhu itapatikana! Hivyo, ipo haja kwa mzazi kufuatilia kwa makini masomo ya mtoto shuleni.”

“Ualimu ni zaidi ya kuwasilisha somo darasani! Mwalimu ni mzazi wa wanafunzi wote, rafiki wa karibu, mlezi wa vipaji na mshauri wa maisha. Siri ya kuwa mwalimu bora ni kuwa kielelezo chema kwa wanafunzi wako,” anashauri.

Joyce alilelewa katika kijiji cha Kariara, eneo la Mukurwe-ini, Kaunti ya Nyeri. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bi Nancy Wamuyu na marehemu Bw Humphrey Mwangi Wambaki.

Mwalimu Joyce Wambui Mwangi wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kariara (1992-2002) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Muruguru Girls, Nyeri (2003-2006) kisha Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Nyeri Vineyards (2008-2010).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kusomea elimu tangulizi kwa watoto (Early Childhood Education) katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Archdiocese of Nyeri Catholic (2011-2013).

Aliyemchochea zaidi kujitosa katika ulingo wa ualimu ni dadake – Jane Mwihaki – ambaye kwa sasa anafundisha katika shule ya upili ya Kiawaithanji, Nyeri. Wengine ni Bi Mugo aliyempokeza malezi bora ya kiakademia shuleni Kariara na Bi Kiama aliyemfundisha katika shule ya sekondari.

Joyce alishiriki mazoezi ya ualimu katika shule ya msingi ya Siema Academy, Nyeri. Aliajiriwa na Nyeri Good Shepherd Academy (2014-2017) kisha akahamia Wima Complex Academy jijini Mombasa mnamo 2018. Amekuwa akifundisha Gilgil Victory Academy tangu Januari 2019.

You can share this post!

Jumwa sasa amrukia Ruto mvutano na Kingi ukizidi

Pingamizi dhidi ya Sonko hazina msingi – Mbogo

T L