MWALIMU WA WIKI: Gikundi mwalimu tajiri wa hamasa

MWALIMU WA WIKI: Gikundi mwalimu tajiri wa hamasa

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU mwenye wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, ana jukumu zito la kuchochea wanafunzi wake kupiga hatua kubwa katika safari ya elimu inayohitaji subira.

Kufaulu kwa mwanafunzi shuleni hutegemea mtazamo wake kwa mwalimu na masomo anayofundishwa. Kwa kuwa uwezo wa wanafunzi wa kumudu masomo hutofautiana, mwalimu anastahili kuelewa kiwango cha kila mmoja wao na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazomwezesha kufikia malengo ya kila kipindi.

Haya ni kwa mujibu wa Bw George Gikundi Murithi ambaye kwa sasa ni mwalimu katika shule ya Ol Joro Orok iliyoko Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua.

“Mwalimu bora huwa karibu na wanafunzi wake na hutia azma ya kufahamu changamoto wanazozipitia shuleni na nyumbani. Anapaswa kuelekeza wanafunzi kwa utaratibu unaofaa na kuwahimiza wajitahidi masomoni,” anasema.

George almaarufu GeeGee alilelewa katika kijiji cha Naari, eneo la Buuri Mashariki, Kaunti ya Meru. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto wawili wa Bw Luka Gikundi Kinoti na Bi Lydia Gatakaa.

Alisomea katika chekechea ya Rugetene, Meru mnamo 1995 kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Muruguma, Meru (1996-2003) kisha shule ya upili ya Ontulili Boys, Meru (2004-2007).

Japo matamanio yake yalikuwa mwanajeshi, alihiari kusomea ualimu (Kiingereza/Fasihi) katika Chuo Kikuu cha Egerton (2009-2013). Aliyemchochea kujitosa katika ulingo wa ualimu ni Bi Lydia Mwenda aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi.

Kabla ya kuhitimu, George alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Njogu-ini iliyoko Tetu, Kaunti ya Nyeri. Alianza kufundisha katika shule ya MCK Michogomone, Meru mnamo 2013. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia katika shule ya Munyange (Nyeri) kisha Kieni iliyoko Subukia, Kaunti ya Nakuru. Aliwahi pia kufundisha katika shule ya Molo Academy, Nakuru mnamo 2015.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri George mnamo 2015 na kumtuma katika shule ya Ol Joro Orok. Mbali na ualimu, amekuwa pia akiwaelekeza wanafunzi wake katika mchezo wa mpira wa vinyoya (Badminton) na kuwashirikisha katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti kwenye tamasha za kitaifa za muziki (KMF).

Kubwa katika maazimio ya George ni kujitosa katika siasa za kitaifa baada ya kuwa mwakilishi na mtetezi wa maslahi ya walimu kupitia vyama vya walimu nchini Kenya. Zaidi ya kuwa mhamasishaji wa masomo ya lugha, anapania pia kujitosa katika uandishi wa kazi bunilizi.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala walimu wengi ambao hutangamana naye katika warsha na makongamano mbalimbali ya kielimu.

Uzoefu anaojivunia katika ufundishaji na utahini umemwezesha kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Kwa pamoja na mkewe Bi Esther Wanjiru, wamejaliwa watoto wawili – Harvey Lucas na Geradine Mukami.

  • Tags

You can share this post!

TALANTA: Pacha waimbaji

Familia ya Assad yapinga faili kufungwa

T L