MWALIMU WA WIKI: Kwa Akinyi ualimu si kazi bali uraibu hasa!

MWALIMU WA WIKI: Kwa Akinyi ualimu si kazi bali uraibu hasa!

NA CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya kuwa na ujuzi wa kufundisha na kipaji cha kutumia vifaa mbalimbali vya ufundishaji, mwalimu bora anastahili kuteka saikolojia ya wanafunzi wake darasani kwa wepesi.

Shughuli za ufundishaji zitakuwa rahisi iwapo mwalimu atasikiliza wanafunzi, kuelewa changamoto zao na kuwaelekeza hatua kwa hatua. Hii ni kazi ngumu inayohitaji moyo na subira.

Aidha, uhusiano wa karibu kati ya mzazi na mwalimu utafunua mengi kuhusu uwezo wa mwanafunzi katika nyanja mbalimbali. Hivyo, mzazi au mlezi ana wajibu wa kufuatilia kwa makini maendeleo ya mtoto wake shuleni.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Mercy Akinyi Onyango anayefundisha katika shule ya msingi ya Missions of Hope Boys iliyoko Ndovoini, Kaunti ya Machakos.

“Mwalimu anastahili kuwa nadhifu na mwenye nidhamu. Awe mchangamfu na ajitume kazini. Atambue mahitaji ya wanafunzi wake, awaelekeze masomoni ipasavyo na awashajiishe maishani,” anaelezea.

Mercy alilelewa katika eneo la Bumala, Kaunti ya Busia. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bw Lucas Onyango na Bi Caroline Atieno.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Bumala (2004-2011) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Bumala (2012-2015) kisha kupokea mafunzo ya kompyuta katika chuo cha Lomati, Bumala (2016).

Japo matamanio yake yalikuwa kusomea masuala ya uanamitindo, alihiari kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John’s Kilimambogo kilichoko Thika (2017-2019).

Maamuzi ya kujitosa katika ulingo wa ualimu yalikuwa zao la kuchochewa zaidi na Bi Ruth Obura aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi ya Bumala.

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo 2019, alipata kazi ya kufundisha katika shule ya msingi ya Hekima Academy iliyoko eneo la Butula, Busia. Alihudumu huko hadi mwaka wa 2021 kabla ya kuhamia Getmore Junior Academy, Kamulu alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Mercy amekuwa akifundisha Kiswahili pamoja na masomo ya Zaraa, Sanaa, Muziki na Sayansi Kimu shuleni Missions of Hope Boys tangu Mei 2022.

Kwa mtazamo wake, mwanafunzi akipata umilisi unaofaa katika stadi mahsusi, atakuwa wa manufaa makubwa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi katika nyanja mbalimbali.

“Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu
kukumbatia matumizi ya mbinu zitakazompa mwanafunzi nafasi maridhawa ya kutononoa vipaji vyake na kuchochea ubongo wake kufanya kazi,” anashauri.

Kubwa zaidi katika matamanio yake ni kujiendeleza kitaaluma na kuweka hai ndoto ya kuwa mhadhiri wa somo la Muziki katika chuo kikuu. Anapania pia kuwa mwandishi maarufu wa diwani za ushairi.

Kufikia sasa, ametunga zaidi ya mashairi 200 anayolenga kuchapisha katika kitabu anachoamini kitabadilisha sura ya ufunzaji na ujifunzaji wa ushairi katika shule za msingi na sekondari ndani na nje ya Kenya.

Mercy pia hushiriki mijadala mbalimbali ya kitaaluma kupitia makongamano na vipindi vya lugha redioni, runingani na mitandaoni. Majukwaa hayo humpa fursa murua za kusambaza maarifa na kutoa mchango mkubwa kuhusu uandishi, utafiti na ufundishaji wa Kiswahili.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kuboresha barabara zinazoelekea kwa mbuga za wanyama...

WANDERI KAMAU: Waraka kwa wanaume: Ni aibu kudhulumu...

T L