MWALIMU WA WIKI: Muthoni ana siri kubwa ya darasa

MWALIMU WA WIKI: Muthoni ana siri kubwa ya darasa

NA CHRIS ADUNGO

MWALIMU mtafiti huwa tajiri wa mbinu mbalimbali za ufundishaji na huelewa kwa mapana kiwango cha mahitaji ya kila mwanafunzi katika darasa lake.

Mwalimu bora anastahili pia kuwa mwajibikaji na mwepesi wa kuelekeza wanafunzi kimaadili huku akichangamkia vilivyo masuala yote yanayohusiana na mtaala.

Haya ni kwa mujibu wa Bi Priscilla Muthoni Chege ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Lugha katika shule ya msingi ya Josnah, Kaunti ya Nairobi.

“Jukumu kubwa la mwalimu ni kuamsha ari ya wanafunzi katika kusoma na kuandika huku akiwahimiza vilevile katika stadi za kusikiliza na kuzungumza,” anatanguliza.

“Hakuna kinachonipa tija katika taaluma ya ualimu kuliko fahari ya kutangamana na watoto wachangamfu kupitia usomaji wa vitabu, michezo, uimbaji, utambaji wa hadithi au shughuli zozote za ufunzaji na ujifunzaji,” anakiri.

Kwa mtazamo wa Priscilla, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo – wa kiwango cha shule za msingi – ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na ni rahisi kuteka saikolojia yao kupitia vifaa vya kidijitali, vibonzo na michoro ya rangi.

“Raha ya mwalimu yeyote aliye na wito wa kufundisha na mapenzi ya dhati kwa taaluma yake, ni kuona mtoto aliyeingia shuleni bila kufahamu chochote akipiga hatua kubwa katika safari ya elimu,” anasema.

“Ualimu ni zaidi ya kuwasilisha masomo ya nadharia darasani. Mwalimu anapaswa pia kutambua na kupalilia vipaji vya wanafunzi wake katika fani mbalimbali huku akiwatia moyo wale wasiokuwa wepesi wa kuelewa mambo anayowafundisha,” anaeleza Priscilla.

Priscilla alilelewa katika eneo la Kigumo, Kaunti ya Murang’a. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa marehemu Bw David Chege na mwalimu mstaafu Bi Esther Nyambura.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Karia-ini, Murang’a (1998–2005) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Bishop Gatimu Ngandu Girls, Kaunti ya Nyeri (2006–2009).

Ingawa ndoto yake ilikuwa kusomea uhasibu, alihiari kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kigari, Kaunti ya Embu (2011–2013). Awali, alikuwa amepokea mafunzo ya udereva na masuala ya kompyuta mjini Murang’a (2009–2011).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Priscilla msukumo wa kusomea shahada ya ualimu (Kiingereza na Fasihi) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kati ya 2015 na 2018. Amekuwa mwanafunzi wa shahada nyingine ya kwanza katika masuala ya usimamizi wa biashara katika Chuo Kikuu cha MKU tangu Septemba 2021.

Baada ya kuhitimu ualimu, Priscilla alianza kufundisha katika shule ya msingi ya Benedito Academy, Murang’a mnamo 2014. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuhamia shule ya msingi ya Josnah. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Lugha mnamo 2017.

Priscilla anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya Kenya. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujikuza kitaaluma na kuwa mhadhiri wa chuo kikuu.

Kwa pamoja na mumwe Bw Jacob Mwangi, wamejaliwa mtoto wa kiume – Wayne Mwangi.

You can share this post!

Serge Gnabry sasa andazi moto jijini Manchester baada ya...

Wakazi wa Kiambu wahimizwa wakumbatie kilimo

T L