MWALIMU WA WIKI: Mwandishi stadi na mlezi wa vipaji

MWALIMU WA WIKI: Mwandishi stadi na mlezi wa vipaji

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA wanafunzi wa madarasa ya chini huelewa mambo wanayofundishwa kwa wepesi, uwezo wao wa kumudu masomo hutofautiana.

Ni wajibu wa mwalimu kufahamu kiwango cha kila mwanafunzi wake na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazomwezesha kufikia malengo mahsusi ya kila mmoja wao.

Mwalimu bora hushirikiana na wanafunzi katika safari ya ufundishaji na ujifunzaji.

Ukaribu huo huwaamshia wanafunzi ari ya kuthamini masomo na kumpa mwalimu fursa ya kutambua vipaji vya wanafunzi wake.

Haya ni kwa mujibu wa mwalimu John Namanda – mwandishi wa vitabu na mlezi wa vipaji ambaye sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Moi Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

“Kigezo cha kutambua mwalimu bora ni uelewa wake wa stadi za mawasiliano na wepesi wake wa kubuni mbinu ainati za ufundishaji,” anatanguliza.

“Mwalimu anastahili kuchochea wanafunzi kutambua umuhimu wa kuwajibika na kujitegemea. Asiwe mwepesi wa hasira, awe mwingi wa stahamala na awahimize mara kwa mara wajitahidi masomoni,” anaeleza.

Namanda alizaliwa mnamo 1987 katika eneo la Lukume, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto sita wa Bi Eunice Luhemba na marehemu Bw Julius Namanda.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Lukume kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Paul’s Emulakha, Kakamega (2005–2008).

Walimu Tom Nyerere, Atibu Bakari na marehemu Ibrahim Abdallah ndio walimvuvia Namanda hamu ya kuzamia taaluma ya ualimu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Wengine ni Bw Ashindu na Bw Ann Mundia waliomnoa vilivyo katika shule ya upili.

Ilikuwa hadi Mei 2010 ambapo Namanda alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Meshad, Kakamega na akafuzu Julai 2012.

Ilhamu ya kutetea Kiswahili ilichangiwa zaidi na Bw Wafula na Bw Kombo – walimu waliomtanguliza vyema katika Fasihi ya Kiswahili na kumpokeza malezi bora ya kiakademia akiwa chuoni.

Namanda alifundisha katika Shule ya Upili ya Lukume (2008–2010) baada ya kukamilisha KCSE. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa la kuzima kiu ya ualimu na kumwamshia hamu ya kuisomea taaluma hiyo.

Baada ya kuhitimu, aliajiriwa na Shule ya Msingi ya Nabongo, Kakamega. Alihudumu huko kwa muhula mmoja pekee kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Fesbeth Academy, Kakamega alikofundisha hadi Disemba 2012 akiwa Katibu wa Idara ya Kiswahili.

Alihamia katika Shule ya Msingi ya Kakamega Hill mnamo Januari 2013 na kuaminiwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Alifundisha huko kwa miaka mitatu kabla ya kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Moi Kabarak mnamo Mei 2016.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni humo Januari 2017.Mbali na kufundisha, Namanda pia ni mtunzi wa mitihani na mwandishi wa kazi bunilizi pamoja na vitabu vya kiada. Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Insha nyingi alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba na za kutamanisha.Amekuwa mtahini wa Baraza la Mitihani ya Kenya (KNEC) tangu mwaka wa 2016.Mnamo 2013, alichapishiwa kitabu cha hadithi ‘Sungura Mjanja’, mwaka mmoja kabla ya kufyatua kitabu kingine cha hadithi ‘Mbweha Mweusi’.

Alishirikiana na Mwalimu Masika, Bw Otieno Mjomba na Bw Zadock Amakoye kuandaa kitabu ‘Fumbuo la Msamiati’ kilichochapishwa na Fumbuo Publishers mnamo 2016.

Kwa pamoja na mkewe Bi Monica, wamejaliwa watoto wanne: Gloria, Gift, Elvins na Adrian Fortune.

You can share this post!

Nyota Shikangwa na Awuor watambulishwa rasmi Uturuki,...

Mudavadi afichua sababu ya kugura OKA

T L