MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mahiri na mwandishi stadi

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mahiri na mwandishi stadi

NA CHRIS ADUNGO

MBALI na majukumu ya kawaida ya kufundisha darasani, yapo mambo mengi ambayo mwalimu anastahili kufanyia wanafunzi wake ndani na nje ya darasa.

Kwa kuwa mwalimu vilevile ni mlezi, inamjuzu kutambua kwamba wapo watoto wanaopitia baadhi ya panda-shuka zilizo na uwezo wa kuwakwaza au kuwazimia mishumaa ya matumaini katika safari ya elimu.

“Kujifunza kusoma na kuandika ni kazi ngumu! Kwa sababu mwalimu anataka wanafunzi wamakinikie stadi hizi, ni muhimu afanye darasa lake kuwa la kusisimua,” anatanguliza Bw Vincent Okwetso ambaye sasa ni mwalimu katika shule ya msingi ya St Anne’s Isibania, Kaunti ya Migori.

“Wape wanafunzi fursa nyingi wazungumzie wanavyojihisi. Mwanafunzi atakuwa mwepesi wa kufichua changamoto anazopitia iwapo mwalimu atamleta karibu na kumfanya rafiki yake. Naye mwalimu atapata fursa ya kubuni mbinu mwafaka za kumchochea kufaulu katika kiwango chake binafsi,” anaongeza.

Bw Okwetso anafarijika kuona mbinu za sampuli hii zikichangia kuchochea wanafunzi kujiamini na kusonga mbele masomoni.

“Kwa kawaida, kusoma na kuandika kunastahili kusisimua na kuchangamsha. Hata hivyo, kuna uwezekano baadhi ya wanafunzi wajenge mitazamo hasi kuhusiana na shughuli hizi za darasani. Ikitokea hivyo, mwalimu huwa na jukumu la ziada la kuamsha ari ya wanafunzi wake,” anaeleza Okwetso.

Kwa mtazamo wake, uzuri wa kufundisha watoto wa umri mdogo – wa kiwango cha chekechea na shule ya msingi – ni kwamba wanaelewa mambo upesi, wana hamu ya kujifunza vitu vipya na wanasahau haraka hata unapowaadhibu kidogo kwa utundu wao.

Okwetso alizaliwa mnamo 1997 katika kijiji cha Mundafi, eneo la Butula, Kaunti ya Busia. Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Esibina mnamo 2004 kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Sikoma kisha D.E.B Mauko, Busia.

Alifaulu vyema katika KCPE na akajiunga na shule ya upili ya Koyonzo Boys, eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega (2012-2015). Alisomea ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST), Kakamega kati ya 2017 na 2021.

Kabla ya kuhitimu chuoni, Okwetso alishiriki mazoezi ya kufundisha katika shule ya upili ya Sigalame, Busia. Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Ilikuwa hadi Januari 2022 alipoajiriwa na shule ya msingi ya St Anne’s Isibania, Kaunti ya Migori kufundisha Kiswahili, Hisabati na Sayansi.

Zaidi ya ualimu, Okwetso pia ni mshairi shupavu na mwandishi stadi wa vitabu vya Kiswahili. Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake katika umri mdogo na aliyetia azma ya kupalilia kipaji hicho ndani yake ni Bw Japheth Okoth aliyekuwa mwalimu wake shuleni Mauko. Mwingine aliyempokeza malezi bora ya kiakademia ni Bw Kilani Misiko aliyemtanguliza vyema katika Fasihi ya Kiswahili.

Okwetso amechangia mashairi mengi katika diwani ‘Lulu za Ushairi’ na ‘Tasnia ya Mashairi’. Baadhi ya tungo zake huchapishwa mara kwa mara katika gazeti la ‘Taifa Leo’ chini ya lakabu ‘Malenga Mkomavu’. Hadithi ambayo amechapishiwa kitabuni ni ‘Lisilobudi’ katika antholojia ya ‘Jirani na Hadithi Nyingine’.

Yeye vilevile hushiriki mijadala ya kitaaluma kupitia makongamano na vipindi vya lugha redioni, runingani na mitandaoni. Majukwaa hayo humpa fursa za kusambaza maarifa na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti na ufundishaji wa Kiswahili.

Miongoni mwa walimu wa Kiswahili wanaozidi kumchochea kitaaluma na kumwelekeza vilivyo katika bahari pana ya utunzi wa kazi bunilizi ni Bw Nashon Kibet na Boaz Aseli almaarufu Ustadh Kipepeo.

You can share this post!

Ruto acheza karata ya mwaniaji mwenza

BURUDANI: Mwigizaji mahiri na mwalimu wa Kifaransa

T L