MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mkuu na mwandishi stadi

MWALIMU WA WIKI: Ni mwalimu mkuu na mwandishi stadi

NA CHRIS ADUNGO

ZAIDI ya kufundisha, mwalimu ana wajibu wa kukuza viwango vya ubunifu miongoni mwa wanafunzi wake na kuwaamshia ari ya kuthamini utangamano.

Shughuli hizo zitakuwa rahisi iwapo mwalimu atateua kutumia mbinu zitakazompa majukwaa anuwai ya kushirikiana vyema na wanafunzi wake kutalii mazingira mbalimbali, kushiriki masimulizi na kufanya kazi ya usomaji katika vikundi.

Kuhusisha wanafunzi moja kwa moja katika shughuli za darasani huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini zaidi. Naye mwalimu atapata nafasi ya kutathmini uwezo wa kila mmoja na kuwaelekeza vilivyo hadi wafaulu katika viwango vyao binafsi.

Haya ni kwa mujibu wa Bw Simon Mwangi ambaye sasa ni Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya Bethlehem Academy, Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

“Siri ya kuchochea wanafunzi kuchapukia masomo ni kuwasikiliza kwa makini, kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwaongoza ipasavyo hatua kwa hatua,” anatanguliza.

“Mwalimu bora anastahili kuwatia shime wanafunzi wasiomudu somo lake kwa wepesi na kuwahimiza wajitahidi zaidi katika hicho wanachopenda kufanya,” anaeleza.

Mwangi alilelewa katika kijiji cha Gatirima, eneo la Ng’arua, Kaunti ya Laikipia. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa Bi Lydia Nyambura na marehemu Bw Cyrus Gatheru.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Gatirima (1981–1988) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Nanyuki High, Laikipia (1989–1992).

Baada kufanya vibarua vya sampuli nyingi katika maeneo ya Laikipia na Kiambu, alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Thogoto, Kaunti ya Kiambu (1997-1999). Alijiendeleza baadaye kitaaluma kwa kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili/Dini) katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kati ya 2014 na 2017.

Mwangi alianza kufundisha Kiswahili, Somo la Jamii na Dini katika shule ya Bethlehem Academy mnamo Machi 2000. Alipanda cheo kuwa Naibu Mwalimu Mkuu mnamo 2001 na akateuliwa kuwa Mwalimu Mkuu mwaka mmoja baadaye.

Zaidi ya kuwaamshia wanafunzi ari ya kuthamini masomo na michezo mbalimbali, aliongoza watahiniwa wake wa 2001 kusajili alama wastani ya 88.2 katika KCPE Kiswahili.

Aliibuka Mwalimu Bora wa Kiswahili katika uliokuwa Mkoa wa Kati mnamo 2002 baada ya wanafunzi wake kuzoa alama wastani ya 83.0 katika KCPE.

Mbali na ualimu, Mwangi pia ni mshairi shupavu na mwandishi stadi wa vitabu vya Kiswahili. Baadhi ya mashairi yake yamekuwa yakichapishwa katika gazeti la ‘Taifa Leo’. Kampuni ya Targeter Publishers ilimchapishia kitabu ‘Msururu wa Targeter Kiswahili kwa Darasa la 7 & 8’ mnamo 2014.

Tajriba pevu anayojivunia katika ufundishaji wa Kiswahili imemfanya mbobevu katika vitengo vyote vya lugha – sarufi, msamiati, ufahamu, ushairi, uandishi wa insha na uchambuzi wa fasihi. Uzoefu huo umemwezesha pia kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Mwangi pia ni mshauri nasaha na mhubiri katika Kanisa la Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA), eneo la Murera, Ruiru.

Kwa pamoja na mkewe Bi Trizah Wahiu, wamejaliwa watoto wanne – Victor Gatheru, Innocent Chege, Ernest Kigotho na Hope Nyambura. Bi Wahiu kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika shule ya msingi ya Magomano, Ruiru.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Bahati aonea soni kovu usoni pa mama

Wakazi wa kaunti 22 wahitaji chakula cha msaada wa dharura

T L