Michezo

Mwamba, Blak Blad na Quins waimarika Kenya Cup Kabras wakisalia kileleni

February 16th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABADILIKO matano yameshuhudiwa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya raga nchini (Kenya Cup) baada ya mechi za raundi ya 14 kusakatwa Februari 15.

Mwamba, Blak Blad na Kenya Harlequin zimepaa nafasi moja kila mmoja, huku Kabras Sugar, KCB na Homeboyz zikisalia katika nafasi tatu za kwanza katika usanjari huo baada ya kupiga Impala Saracens 37-26, Nakuru 31-18 na Menengai Oilers 37-14 mtawalia, ugenini.

Mabingwa wa mwaka 1983 Mwamba walipepeta wenyeji Kisumu 50-32 uwanjani Mamboleo na kurukia nafasi ya sita kutoka nambari saba. Wana alama 34, moja mbele ya washindi wa mwaka 2013 na 2014 Nakuru, ambao wametupwa nafasi moja nje ya sita-bora baada ya kucharazwa 31-18 na mabingwa watetezi KCB mjini Nakuru.

Wafalme wa mwaka 2016 Kabras wanaongoza kwa alama 65 na wamo mbio tena kuandaa fainali za ligi hii ya klabu 12 kwa mwaka wa pili mfululizo. Mshindi wa ligi katika kipindi cha kawaida huwa mwenyeji wa fainali. Mshindi huyo pamoja na nambari mbili huingia nusu-fainali moja kwa moja, huku nambari tatu hadi sita wakipigania tiketi zingine mbili za kushiriki nusu-fainali.

Kwa sasa, KCB inapumua nyuma ya Kabras kwa kujizolea alama 64 ikifuatiwa na Homeboyz (59), Impala Saracens (42) na Oilers (36). Kabras, ambayo imeshiriki nusu-fainali zote tangu iingie Ligi Kuu mwaka 2014, ilibwaga Impala japo kwa jasho 37-26 Jumamosi. Vita vya kumaliza msimu wa kawaida katika nafasi za tano na sita vinahusisha Impala, Oilers, Mwamba na Nakuru.

Zikisalia mechi mbili msimu wa kawaida utamatike, Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta haiwezi kuingia mduara wa sita-bora. Hata hivyo, Blak Blad imejihakikishia msimu mwingine kwenye Ligi Kuu baada ya kunyamzisha mabingwa wa mataji 17 Nondescripts 32-17 katika ardhi yao ya Jamhuri Park.

Blak Blad iko katika nafasi ya nane kwa alama 23. Imeruka juu nafasi moja, sawa na mabingwa wa zamani Kenya Harlequin waliolima Western Bulls 28-16 na kukalia nafasi ya tisa. Quins ina alama 22.

Nondies inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 17, nne pekee nje ya maeneo hatari ya kutemwa. Bulls na Kisumu zinapatikana katika nafasi mbili za mwisho za kushushwa ngazi. Bulls ina alama 13 nayo Kisumu imekusanya alama sita.

Matokeo (Februari 15): Top Fry Nakuru 18-31 KCB

Menengai Oilers 14-37 Homeboyz

Western Bulls 16-28 Kenya Harlequins

Impala Saracens 26-37 Kabras Sugar

Nondescripts 17-32 Blak Blad

Kisumu 32-50 Mwamba