Michezo

Mwamba RFC kukosa uwanja wa nyumbani

September 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MOJAWAPO ya klabu kongwe zaidi za raga ya humu nchini, Mwamba RFC, sasa haitakuwa na uwanja wa nyumbani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 42.

Kikosi hicho ambacho kimekuwa kikijiendeshea shughuli zake katika uga wa Nairobi Railways Club tangu 1977, sasa itaondoka uwanjani humo kupisha shughuli za kujengwa kwa kituo cha mabasi na Barabara Kuu kutoka eneo la Westlands hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Kwa mujibu wa Caleb Musamali ambaye ni meneja wa Nairobi Railway Club, baadhi ya sehemu zitakazoathiriwa na ujenzi huo uwanjani humo ni kitengo kilichokuwa kikitumiwa kwa minajili ya mchezo wa soka, raga na maonyesho ya magari ya kuuzwa.

Mwamba RFC walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya Cup kwa mara ya kwanza na mwisho mnamo 1983. Hata hivyo, klabu hiyo imekuwa ngome ya wanaraga wa haiba kubwa ambao wameishia kuacha kumbukumbu za kudumu katika mchezo huo baada ya kutamba katika vikosi vya taifa.

Kati ya wachezaji wa haiba kubwa ambao wamewahi kupokezwa malezi ya raga kambini mwa Mwamba RFC ni Edward Rombo, Collins Injera na Humphrey Kayange.

“Jengo Kuu la klabu halitaathiriwa wala kubomolewa kwa sababu lina historia ndefu na kumbukumbu za kudumu,” akasema Musamali kwa kusisitiza kwamb serikali kupitia Wizara ya Usafiri, ilijipatia umiliki wa shamba hilo kutoka kwa chama cha wafanyakazi wastaafu wa Kenya Railways mnamo 2006.

“Shughuli nzima imepitia mchakato wa kisheria na hakuna lolote tunaloweza kufanya kwa kuwa Mwamba RFC hawakuwa na stakabadhi za kuonyesha mwafaka waliokuwa nao na chama hicho cha wafanyakazi wastaafu kuhusu jinsi ya kutumia uwanja huo wa Nairobi Railways Club.

“Ni uchungu sana kwa kikosi kupoteza uwanja ambao wameuita wao wa nyumbani kwa kipindi kirefu cha miongo kadhaa. Uwanja ambao umelea baadhi ya wanaraga maarufu zaidi duniani kwa sasa,” akasema Rais wa Mwamba RFC, Alvas Onguru.

“Ni bahati tu kwamba hakuna raga inayochezwa kwa sasa baada ya Serikali kusitisha shughuli zote za michezo mnamo Machi 2020 ili kukabiliana na msambao wa virusi vya corona. Sasa tuna ulazima wa kutafuta uwanja mpya wa nyumbani, akaongeza Onguru kwa kutaka serikali iwasaidie kutafuta makao mapya yakayohifadhi kikosi chao.

“Hii ni klabu ya kwanza ya jamii iliyowapa chipukizi wa kike na kiume wa humu nchini fursa ya kung’arisha nyota zao katika raga na taaluma nyinginezo,” akaelezea Onguru.