Habari

Mwamko mpya watoto wakianza mtihani wa kitaifa

September 15th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

SEKTA ya elimu nchini inatarajiwa kuweka historia Jumatatu wakati wanafunzi wa Darasa la Tatu watakapofanya mtihani wa kitaifa kwa mara ya kwanza.

Hisia mseto zimezidi kutolewa na wadau kuhusu mtihani huo ambao Wizara ya Elimu inasisitiza hautakuwa na ushindani kama Mitihani ya Kitaifa ya Shule za Msingi na Upili (KCPE na KCSE), hivyo basi hakuna haja wanafunzi na walimu kuwa na wasiwasi.

Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Walimu wa Shule za Msingi (KEPSHA) Bw Nicholas Gathemia alisema kuwa wanachama wao walishirikiana na serikali kuhakikisha changamoto zinazotarajiwa kuathiri shughuli hiyo ya kihistoria zimetatuliwa.

“Ni kweli kuna matatizo madogo madogo ambayo tumepokea. Hata hivyo, lazima ikumbukwe kwamba hii ni mara ya kwanza ambapo wanafunzi wanafanya mtihani huu. Ni imani yetu kuwa hali itakuwa tofauti kwa awamu ijayo,” akasema kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (KNPA) Bw Nicholas Maiyo, aliyewashauri wazazi kushirikiana na walimu kuhakikisha kuwa mazingira ya wanafunzi kufanya mtihani huo yanafaa.

“Huu ni mfumo mpya wa utahini. Tunatarajia ukumbwe na changamoto kadhaa. Ombi letu ni kwa wizara kuzingatia malalamishi ya wazazi, ikiwa mazingira ambayo wanafunzi walipo yanahitaji kuangaliwa upya,” akasema.

Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kimekuwa mstari wa mbele kikisisitiza kuwa mfumo huo haufai kwa wanafunzi.

Katibu Mkuu wa KNUT anayekumbwa na upinzani Bw Wilson Sossion alisema kuwa baada ya utafiti wao, walibaini kuwa, walimu hawakupata mafunzo ya kutosha, hivyo ni mapema kuanza kuutekeleza.

Lakini Waziri wa Elimu Prof George Magoha anashikilia kwamba mfumo huo ni “kama meli ambayo imeng’oa nanga” hivyo hakuna anayeweza kuingilia utekelezaji wake.

Kulingana na wataalamu, maandalizi ya mtihani huo ndicho kibarua cha kwanza dhidi ya serikali kuhusu ufaafu wa mfumo mpya wa elimu.

Wanafunzi 1.3 milioni wanaotarajiwa kufanya mtihani huo utakaokamilika Ijumaa.

Wadau wengi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walieleza kwamba ingawa mfumo wa elimu wa umilisi na utendaji utawafaa sana wanafunzi, mtihani huo uliharakishwa sana.

Uchunguzi wa kina ‘Taifa Leo’ pia umebaini kuwa baadhi ya shule hazina vifaa vya kutosha, licha ya hakikisho kutoka kwa Wizara ya Elimu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC), Bi Mercy Karogo alisema kuwa walichukua hatua hiyo baada ya baadhi ya shule kutimiza masharti yote yaliyotakinana na baraza hilo.

“Tuliziruhusu shule ambazo zilikuwa zishakamilisha matayarisho yake kuanza kuwatahini wanafunzi wao mapema kwa majaribio. Hili litawapa nafasi ya kuwa na uelewa wa kina kuhusu masuala wanayohitaji kuchukua muda zaidi ili kuyaelewa vizuri,” akasema Bi Karogo.

Baadhi ya walimu wakuu walisema kuwa hawajui namna ya kutoa mwongozo wa mtihani huo kutoka kwa tovuti ya KNEC.

Usajili wa mitihani hiyo umekuwa ukiendelea tangu Julai 12, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoufanya wamesajiliwa.

Bi Jane Mwamburi, ambaye ni mzazi katika Shule ya Msingi ya Mwiki, Kaunti ya Nairobi, alisema kuwa wazazi wengi wamo kwenye giza kuhusu masuala ambayo watoto wao watatahiniwa.

“Nimekuwa nikimsaidia mwanangu kufanya mazoezi tendaji anayopewa na mwalimu wao. Hata hivyo, wengi wetu hatujui kile ambacho watatahiniwa,” akasema.

Wazazi wengine pia walisema kuwa ingawa wanaunga mkono mageuzi ya mfumo wa elimu, serikali haingeharakisha kuwatahini wanafunzi kabla ya kutatua changamoto za kimiundomsingi zinazozikumba shule nyingi.

Baadhi ya walimu wakuu pia wamelalamika kuwa shule zao zimo katika maeneo ambayo hayana mtandao wa intaneti, hali ambayo inawalazimu kutumia pesa nyingi kusafiri safari ndefu katika maeneo yaliyo nao.