Mwana anaswa kwa mauaji ya watu 5 wa familia yake

Mwana anaswa kwa mauaji ya watu 5 wa familia yake

Na BENSON MATHEKA

MAAFISA wa upelelezi jana walimkamata mshukiwa mkuu anayehusishwa na mauaji ya watu watano wa familia moja Kaunti ya Kiambu, yaliyotokea siku nne zilizopita.

Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), ilisema maafisa wake walimkamata Lawrence Simon Waruinge, mwana wa mfanyabiashara aliyeuawa pamoja na mkewe, watoto wao wawili na mfanyakazi wao.Mshukiwa mwenye umri wa miaka 22, alikamatwa katika maficho yake eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu.

Baada ya kuhojiwa, jana mchana, mshukiwa aliwapeleka wapelelezi hadi Naivasha ambapo walipata silaha zilizotumiwa kuwaua watu hao.“Mshukiwa ambaye ni kifungua mimba wa familia hiyo na mwanafunzi wa chuo kikuu kimoja cha kibinafsi, alikamatwa katika maficho yake eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu,” DCI ilisema kwenye taarifa.

DCI pia ilisema kwamba wapelelezi walimkamata mwanamke anayeaminika kuwa mpenzi wa mshukiwa huyo anayefanya biashara katika mtaa wa Biafra mjini Thika.

Polisi pia wanaamini kwamba mshukiwa alishirikiana na watu wengine watano kumuua baba yake Nicholas Njoroge Warunge, mkewe Annie, watoto Christian na Maxwell pamoja na mfanyakazi wao James Kinyanjui.Lawrence alitoweka baada ya watano hao kuuawa kikatili na polisi wakashuku alikuwa mshukiwa mkuu.

Awali, polisi walisema kwamba walifuatilia simu yake hadi Naivasha, kabla ya kupatikana Thika na kisha Kabete alikokamatwa Ijumaa. Duru za polisi zilisema kwamba mshukiwa alienda kwa jamaa zake wanaoishi eneo hilo kujificha kabla ya kutiwa mbaroni.

Eneo la uchunguzi. Picha/ Hisani

Wapelelezi walisema kwamba mshukiwa aliwapeleka Naivasha ambapo walipata silaha zilizotumiwa kutekeleza mauaji hayo katika juhudi za kubaini watu hao walivyouawa.

Polisi walielekeza uchunguzi kwa watu wa familia baada ya kugundua kwamba nyumba ambayo miili ya waathiriwa ilipatikana haikuwa imevunjwa.

Waruinge alikuwa amewasili Kenya kutoka Amerika anakofanya kazi. Mshukiwa anazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea.Mwili wake Njoroge ulipatikana nje ya nyumba ilhali ya wengine ilipatikana ndani ya nyumba Jumatano asubuhi.

Polisi wanashuku mauaji hayo yalisababishwa na mzozo wa kifamilia.Duru zinasema mnamo Desemba mshukiwa alikuwa ameripoti kwa chifu kwamba wazazi wake walikuwa wachawi.

Baadaye, mama yake alienda kumchukua kutoka ofisi za chifu akidai alikuwa na matatizo ya akili. Mama yake ni mmoja wa waliouawa.Haikubainika alivyofika Naivasha baada ya mauaji hayo kabla ya kusafiri hadi Thika na baadaye Kabete alikokamatwa.

Mkuu wa polisi kaunti ya Kiambu Ali Nuno alisema wanachunguza mauaji mengine ambayo yalitokea katika familia hiyo awali kubaini iwapo yanahusiana na ya majuzi.Alisema mauaji ya Jumatano ni ya tano katika familia ya mshukiwa tangu 2016.

You can share this post!

Uhuru anguruma, aashiria atamruka Ruto urais 2022

Ruto ashauriwa kuungana na Kalonzo kupenya Ukambani