Habari Mseto

Mwana wa mbunge afariki katika kisa kinachotajwa ni kujitoa uhai

March 1st, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

MWANA wa kiume wa mbunge wa Bomet Magharibi, Beatrice Kones akifahamika kama Collins Kipyegon amefariki katika kisa kinachochunguzwa na kinachotajwa kwamba huenda alibugia sumu.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Kaunti ya Bomet, Naomi Ichami, kijana huyo aliaga dunia alipokuwa akipokezwa
matibabu ya kunusuru uhai wake katika hospitali ya Nakuru War Memorial.

“Mauti hayo yalianza kama mzaha tu ambapo alipachika ujumbe katika mtandao wa kijamii kuwa alikuwa akihisi kujiua. Kabla ya wandani wa familia hiyo kupata ujumbe huo ambao ulikuwa umewekwa katika ukurasa wake wa Facebook mnamo Alhamisi, tayari mambo yalikuwa yameshavurugika,” akasema Bi Ichami ambaye aliongeza kuwa tukio hilo linachunguzwa.

Ni kisa kilichotokea katika makazi ya kijana huyo katika mtaa wa Ngata.

Mwendazake alikuwa na umri wa miaka 39 na marafiki zake baada ya kuusoma ujumbe wake katika ukurasa wa Facebook na wakawahi kumjulia hali walimpata akiwa hoi na walipomfikisha hospitalini, aliaga dunia.

Tayari, mamake ambaye alikuwa katika ziara rasmi katika taifa la Afrika Kuisni imeripotiwa aliabiri ndege kurejea nyumbani ili
kuomboleza kifo cha mwanaye wa tatu katika familia ya watoto watano.