Habari Mseto

'Mwanachuo alidungwa mara sita shingoni na tumboni hadi kufa'

May 26th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Mahakama kuu ya Nakuru Alhamisi ilipokezwa ripoti ya upasuaji wa mwili wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Egerton, aliyedaiwa kuuawa na mpenzi wake baada ya ubishi mwezi Februari.

Akifikisha ripoti ya upasuaji wa mwili wa marehemu mbele ya jaji Joel Ngugi Alhamisi, daktari wa upasuaji katika hospitali ya Nakuru Level Five Titus Ngulungu alieleza korti kuwa alipofanya upasuaji alibaini kuwa marehemu, Bi Cynthia Chelagat alifariki kutokana na kudungwa kisu mara kadhaa shingoni na damu iliyotiririka kwa wingi kuziba mishipa ya hewa.

Bi Chelagat alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo hicho na aliuawa mnamo tarehe 19 Februari katika chumba alichokuwa akiishi nje ya chuo.

Dkt Ngulungu alieleza korti mwili wa marehemu ulikuwa na zaidi ya majeraha sita, yakiwemo shingoni, tumboni na kwenye akili.

“Kutokana na majeraha, damu ilitiririka hadi kwenye mapafu na kuziba mishipa ya damu na hivyo hewa ikakosekana mwilini. Aidha, akili ziliadhirika na ukosefu wa hewa baada ya mishipa kujeruhiwa,” Dkt Ngulungu akaeleza korti.

Kulingana na daktari huyo, majeraha mengine kwenye magoti na vidole vya marehemu yalionyesha namna alivyokuwa akipambana na muuaji.

Mshukiwa, Bw Edmond Ruto, ambaye alikuwa mpenzi wake marehemu yuko rumande baada ya kushindwa kulipa dhamana aliyopewa na korti ya pesa taslimu Sh300,000.

Daktari huyo ni mmoja wa mashahidi wanne wa upande wa mashtaka ambao wameorodheshwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Kiongozi wa mashtaka aliomba korti kuahirisha kesi kwani vifaa Fulani ambavyo mashahidi wengine wanategemea ili kutoa ushahidi wao bado havijatolewa kwenye maabara ya serikali.

Kesi hiyo ilipewa tarehe saba na nane Novemba kusikizwa, lakini itatajwa Julai 18.