Habari Mseto

Mwanachuo auawa na wenzake akijaribu kuvunja ofisi

January 15th, 2019 1 min read

Na Steve Njuguna

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Laikipia Jumapili alipigwa hadi kufa na wanafunzi wenzake katika bewa kuu la chuo hicho mjini Nyahururu, Kaunti ya Laikipia.

Kulingana na OCPD wa Nyandarua Kaskazini, Timon Odingo, mwanafunzi huyo aliyetambuliwa kama Joseph Moseti, 30, alifumaniwa akijaribu kuvunja mlango wa ofisi ya Makamu Chansela ndipo akapigwa na wenzake hadi akafa.

“Alikamatwa na walinzi wa chuo akijaribu kuingia ofisi ya naibu chansela kwa kuvunja mlango. Hata hivyo walinzi hao walishindwa kumwokoa walipozidiwa na umati wa wanafunzi waliompiga marehemu hadi akafariki,” akasema Bw Odingo.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi wamejitokeza kukanusha kuhusika na kifo cha marehemu na kusema kwamba walinzi hao ndio walimpiga mwenzao hadi kufa.

“Usimamizi wa chuo lazima ujitokeze na kuyaweka mambo bayana,” akasema mwanafunzi moja ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

Chama cha wanafunzi chuoni humo hata hivyo hakikuweza kufikiwa ili kupata kauli yao.

Mwili wa mwendazake ulipelekwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Nyahururu.