Habari Mseto

Mwanachuo Rita Waeni hatimaye azikwa katika hafla fupi nyumbani kwao

February 5th, 2024 1 min read

BENSON MATHEKA Na PIUS MAUNDU

RITA Waeni, msichana aliyeuawa katika makazi ya muda mfupi mtaani Roysambu wiki tatu zilizopita, amezikwa.

Mazishi hayo yalifanyika katika Kijiji cha Mukimwani, Kaunti ya Makueni Jumatatu, Februari 5, 2024 katika hafla iliyohudhuriwa na jamaa zake wa karibu pekee.

Maafisa wa polisi waliokuwa na silaha waliweka ulinzi mkali karibu na lango la boma kuwazuia wanakijiji.

Waandalizi wa mazishi hayo walikuwa wametangaza wazi kuwa ni jamaa wa karibu tu ndio wangeruhusiwa kuingia katika eneo la mazishi hayo, mtu wa familia aliyehudhuria mazishi hayo aliambia Taifa Leo.

Mchungaji Fred Auma wa Kanisa la Ridgeways Baptist jijini Nairobi aliongoza hafla ya mazishi iliyochukua saa mbili kuanzia saa nne asubuhi.

Ilitawaliwa na mito ya kutaka haki itendeke.

“Tuna amani kwa sababu tunajua kwamba familia yetu kubwa, marafiki, wafanyakazi wenzetu na Wakenya wengi wataelewa uamuzi huu,” Lillian Mutea, shangazi ya Waeni na msemaji wa familia, alisema katika kikundi cha

WhatsApp kilichoandaa mazishi.

“Tunamshukuru kila mtu kwa msaada wake, michango na kwa kutuombea kila mara. Pia tunawakaribisha wale ambao wanaweza kutaka kutoa rambirambi zao kwa wazazi wa Waeni kuendelea kufanya hivyo,” aliandika.