Habari za Kaunti

Mwanadada adaiwa kujitia kitanzi kwa kukosa kazi

January 10th, 2024 1 min read

NA KASSIM ADINASI

KIJIJI cha Umiru kilichoko Yala katika Kaunti ya Siaya kinaomboleza baada ya mmoja wao kupatikana akiwa ameaga dunia kwa kile kinadhaniwa ni kujitia kitanzi.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya polisi inayoeleza kwamba mwili wa Vera Amondi Okoth aliyekuwa na umri wa miaka 27, ulipatikana ukining’inia ndani ya bafu huku kamba ikiwa shingoni.

Inadaiwa kwamba mwanadada huyo kabla ya kuchukua hatua hiyo, alikuwa amelalamika kwamba kati ya maombi 500 aliyotuma kutafuta ajira, hakuna kazi hata moja aliyoitiwa.

Ripoti ya polisi inasema mamake alienda kumuamsha asubuhi chumbani mwake lakini hakumkuta. Alifululiza hadi katika bafu na akashtuka kukumbana na mwili wa binti yake.

“Mama ya Vera Amondi Okoth alienda kumuamsha lakini dalili ikawa wazi kwamba hakuwa chumbani, hivyo kuenda kwa bafu akakumbana na mwili ukining’inia,” inasema ripoti hiyo ambayo Taifa Leo imeona.

Polisi kutoka Yala walipofika eneo la tukio, walipata mwili huo na kuukagua, waliona kwamba haukuwa na majeraha ya wazi.

Baada ya hayo kutokea, imeripotiwa kwamba msichana huyo alikuwa amemuuliza mamake kama kweli ingetokea siku moja akawa na bahati ya kupata kazi.

Polisi pia waligundua kwamba alikuwa na shahada ya Digrii ya Sayansi aliyotunukiwa mwaka 2019 kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST).

Japo hakuna kijikaratasi chochote alichokiacha akielezea sababu ya kujitoa uhai, vyeti vyake vilipatikana kitandani.

Mwili unahifadhiwa katika mochari ya Siaya kusubiri kufanyiwa upasuaji.