Habari za Kaunti

Mwanafunzi ajitia kitanzi kwa kuachwa na mpenziwe

March 26th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MWANAFUNZI wa kiume wa Chuo Kikuu cha Kisii amepatikana akiwa amefariki dunia katika nyumba ya kupanga mtaani Gekomu katika eneobunge la Nyaribari Chache.

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu, alikuwa na umri wa miaka 23. Ni wa Kitivo cha Sayansi ya Wanyama chuoni.

Mwili wake ulipatikana ukining’inia kutoka kwa paa la chumba chake Jumanne asubuhi kulingana na naibu chifu wa Kiamabundu John Ondande.

Kulingana na Bw Ondande, mwanafunzi huyo kabla ya kujitoa uhai alimtumia rafiki yake ujumbe mfupi wa simu (SMS) akimjulisha kuwa aliamua kujitoa uhai kwa sababu mpenzi wake alikuwa amekatiza uhusiano wake naye.

Wakazi wa Gekomu, Kisii wakiwa karibu na eneo la tukio ambapo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kisii alipatikana amefariki dunia ndani ya chumba chake. Inadaiwa marehemu alichukua hatua hiyo baada ya kuachwa na mpenziwe. Naibu Chifu wa Kiamabundu John Ondande amethibithisha tukio hilo. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Chifu huyo aliongeza kuwa Jumatatu jioni, majirani walimwona akiharibu kipakatalishi chake kama njia mojawapo ya kudhihirisha hasira zake.

“Majirani walimwona akiharibu laputopu yake. Aliivunja ikawa vigae vidogovidogo,” Bw Ondande alisema.

Chifu huyo aliwasihi vijana wa sasa kutochukulia mahusiano yaanziayo vyuoni kwa uzito kwani chochote chaweza kutokea.

“Ushauri wangu kwa vijana hasa walioko katika vyuo vikuu, ni kwamba waache kuweka zingatio kwa mahusiano ya kimapenzi wanapokuwa katika taasisi hizo. Usimpende mtu kiasi kwamba unajitoa uhai ikitokea kwamba mnaachana. Mpenzi mwingine akikuacha, salia thabiti kwa kuwa Mungu ana mtu mahali pengine kwa ajili yako,” Bw Ondande akashauri.

Aliongeza, “Kwa kina dada, ikiwa umeamua kuachana na mtu, tafadhali acha kumtumia arafa za kumdhihaki, ambazo zinaweza kumpa kijana wa kiume msongo wa mawazo. Ikiwa umeamua kuachana naye, fanya hivyo kwa busara.

Familia ya mwendazake ambaye anatoka Kenyenya imeambiwa kuhusu kilichojiri kabla ya mwili kupelekwa katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii.