Habari Mseto

Mwanafunzi ajiua mamake kumkera kwa kudai anagawa uroda kijijini

April 10th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO na GERALD BWISA

MWANAFUNZI wa darasa la sita katika kaunti ya Trans Nzoia alijitia kitanzi baada ya mama yake kudai alikuwa na mazoea ya kushiriki ngono na wavulana kijijini.

Mercy Gathoni, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Tuwani, alipatikana akining’inia kwa paa ya chumba chake cha kulala alichokodisha katika kitongoji cha Tuwani Jumapili jioni.

Naibu wa chifu, Jackline Sitoya alisema kuwa mwanafunzi huyo wa miaka 13 aliacha kijikaratasi kwa kitanda chake kilichosema kuwa alijitoa uhai kwa kuwa mamaye alikuwa akimsingizia kushiriki tendo la ndoa  na wavulana wa kijiji hicho.

“Mwanafunzi huyo alikorofishana na mamaye baada ya kushuku kuwa mwanawe alikuwa akiwalisha uroda wavulana kijijini, jambo ambalo lilimkera Gathoni,” akaambia Taifa Leo.

Mamaye hakuwepo wakati kisa hiki kilitendeka. Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kitale.