Habari Mseto

Mwanafunzi aliyejitolea kumtunza mamaye mlemavu apunguziwa mzigo

April 2nd, 2018 2 min read

NA PETER MBURU

MTOTO wa miaka kumi ambaye aligonga vichwa vya habari mwishoni mwa Machi kwa kumsaidia mamake mlemavu kwa kumsukuma kwenda kazini kabla ya kwenda shuleni kila siku na kufanya kazi nyingine nyingi za kinyumbani, huku akiathirika kimasomo  sasa anaweza kutabasamu baada ya kilio chake kusikika na wahisani.

Kevin Momanyi, mtoto wa darasa la nne kutoka mtaa wa Shabaab, Nakuru alitoa kafara kubwa ya maisha yake ili kuhakikisha kuwa mamake, pamoja na familia zima wanasaidika.

Hata hivyo, juhudi zake za kuamka saa kumi usiku kuanza kazi za nyumbani ili kumsaidia mamake Irene Monari, 32, ambaye ni kiwete ziliishia kudororesha elimu yake, jambo lililoangaziwa na Taifa Leo.

Mbunge wa kuwakilisha watu wenye ulemavu, Bw David Ole Sankok asema na Bi Monari wakati alipomtembelea na mwanawe. Picha/ Peter Mburu

Alhamisi, kilio cha mtoto huyo kilisikika baada ya mbunge wa kuwakilisha watu wenye ulemavu nchini Bw David Ole Sankok kutembelea familia hiyo.

Bw Sankok aliipa msaada familia hiyo kwa kulipa karo ya watoto, kuwapa vyakula na kumwahidi Bi Monari kazi katika Ikulu ya Rais, Nakuru ili aondokee matatizo mengi.

“Huyu mama ni shujaa kwa kuwa hata akiwa mlemavu hakwenda barabarani kuomba wala kuwatumia wanawe bali amejifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa wanapata elimu bora. Walemavu wanahitaji kupewa nafasi, sio kuhurumiwa,” akasema mbunge huyo.

Aidha, ushujaa wa mtoto huyo wa miaka kumi ulitambuliwa kwa kina, na hatimaye akiondolewa mzigo mkubwa ulioelekea kuangamiza mustakabali wake.

Bi Irene Monari ahutubia umati uliokusanyika kushuhudia maisha yake yakibadilika. Picha/ Peter Mburu

“Huyu ni mtoto shujaa kwani badala ya kuaibikia hali ya mamake na kumkana kama wanavyofanya wengi, aliamua kumsaidia, hata kama hatua zake zilikua zikimwadhiri vikubwa,” akasema Bw Sankok.

Mbunge huyo alisema historia ya walemavu nchini imetoka mbali, tanzia wakati watoto walipokuwa wakiuawa walipozaliwa na ulemavu, hadi sasa ambapo serikali imewatambua na kuwaheshimu.

Walimu, majirani na jamii nao walisifu mtoto huyo shujaa, ambaye katika elimu amejitunukia sifa tele.

“Mtoto huyu akipewa nafasi ya kusoma na kushiriki utoto wake ana nafasi nzuri kufanya vyema katika elimu,” akasema mwalimu mkuu wa shule anayosomea mtoto huyo, Dennis Seko.