Habari Mseto

Mwanafunzi aliyesaidiwa na shirika la Nation Media kupata ufadhili afaulu kuzoa alama A

January 8th, 2024 2 min read

NA STANLEY NGOTHO

Mwanafunzi mwerevu kutoka kwa familia isiyojiweza mjini Kitengela aliyesaidiwa na shirika la Nation Media Group mnamo 2020 amefaulu kujipatia alama ya A kwenye matokeo ya KCSE yaliyotolewa Jumatatu.

Shadrack Mithamo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 14 alikuwa amefaulu kujipatia alama 416 kwenye mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) 2019 lakini mamake, ambaye ni mzazi wa kipekee alishindwa kumpeleka kujiunga na Shule ya Upili ya Lenana aliyoitwa. Ni jambo lililomfanya kuanza kufunga na kuomba akitaka Mungu afungue milango ya usaidizi.

Mithamo, anayetokea kijiji cha Noonkopir, Kitengela, Kaunti ya Kajiado alikuwa anatembea kwa umbali wa kilomita 12 kila siku kwenda kaunti jirani ya Machakos akisoma shule ya msingi.

Hata hivyo, NMG iliangazia masaibu yake na mfadhili alijitokeza na kumsaidia kujiunga na Shule ya Lenana.

Jumatatu, Januari 8, 2024 saa moja baada ya Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kutangaza matokeo ya KCSE ya 2023, Nation ilimfikia akiwa na mamake mjini Kitengela. Kijana huyo aliyekuwa amevalia tishati nyeupe, kinyasa cha kijivu na champali aina ya crocs za samawati alikuwa mwingi wa tabasamu. Alipata A yenye pointi 83.

Aliambia Nation kwamba ufanisi wake ulichochewa na ari ya kutoangusha wahisani wake. Anasema alitaka kupata alama nzuri hata zaidi na kwamba angependa kusomea uhandisi wa programu za kompyuta katika chuo kikuu.

“Bado nakumbuka kama jana, siku ambayo Nation ilinisaidia kupata mdhamini nikajiunga na shule ya upili. Mimi na mamangu tulilia usiku kucha na niliapa kwamba sitajiangusha wala kuangusha wahisani wangu. Nataka niende chuo kikuu ili siku moja nimsaidie mamangu na jamii iliyonilea,” akasema Mithano.

Miaka minne iliyopita alikuwa ameambia Nation kwamba angependa kusomea urubani wa ndege lakini huenda sasa amebadili nia na kutaka kusomea uhandisi.

Mamake, Eunice Mbithe hangeweza kuficha furaha yake akimpongeza mwanawe kwa kazi nzuri aliyofanya ya kupita mtihani wake.

“Leo ndio siku nzuri zaidi katika maisha yetu hapa kama familia. Hatuna vitu vingi maishani lakini Mungu amejibu maombi yetu. Nashukuru Tumaini (shirika lisilo la kiserikali lililomlipia karo) na Nation media Group kwa kutusaidia,” akasema Bi Mbithe akibubujikwa na machozi ya furaha.

Mama huyo hufanya kazi za kijungujiko kulisha familia yake. Familia hiyo kwa sasa imepewa makao na mhisani katika mji wa Kitengela.

  • Imetafsiriwa na FATUMA BARIKI 

[email protected]