Mwanafunzi amtandika mwalimu katika fumanizi la uroda darasani

Mwanafunzi amtandika mwalimu katika fumanizi la uroda darasani

DONNA ATOLA na DICKENS WASONGA

MWALIMU wa shule ya upili katika Kaunti ya Busia anauguza majeraha baada ya kushambuliwa na mtahiniwa wa kiume wa Kidato cha Nne (KCSE) alipomfumania akifanya mapenzi na mwenzake wa kike darasani.

Polisi walisema mwalimu huyo alipigwa na mwanafunzi huyo mvulana muda mfupi baada ya kufanya mtihani wa somo la Baiolojia mnamo Ijumaa

“Baada ya mtihani wa somo la Baiolojia nilizunguka madarasani ndiposa nikapata mwanafunzi huyo akiwa amempakata mwenzake wa kike mapajani. Niliwakaripia na kuwataka kuacha tabia hiyo,” alisema mwalimu huyo aliyeomba jina lake libanwe.

Alisema wawili hao waliendelea kupapasana hata baada ya kuwaonya.

“Ghafla, mtahiniwa wa kiume alinirukia na kuanza kunipiga na kuniumiza mdomoni na puani,” alisema mwalimu.

“Wasimamizi wa mtihani waliokuwa karibu walikuja kuniokoa baada ya kusikia kelele. Walinitoa nje ya darasa na kunipeleka hospitalini. Nilitibiwa katika hospitali ya kaunti na nikaruhusiwa kwenda nyumbani,” aliongeza.

Katibu wa Chama cha Walimu (Kuppet,) tawi la Busia, Bw Mophat Okisai alishutumu kitendo hicho akisema kuwa hiyo ilikuwa ishara kwamba usalama wa walimu umezorota shuleni.

“Kisa hicho kimetushtua na hiyo ni ishara tosha kwamba walimu si salama shuleni. Wanafunzi wanafaa kuchagua kati ya kuwa wahuni au wanafunzi,” alisema Bw Okisai.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Busia, Jacob Narengo, alisema mtahiniwa huyo alikamatwa.

Bw Narengo, hata hivyo, alisema mtahiniwa huyo ataruhusiwa kufanya mitihani iliyosalia kabla ya kufikishwa kortini kujibu mashtaka ya kumshambulia mwalimu.

Kwingineko, mtahiniwa katika shule ya Upili ya Member iliyoko eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya alizimia na kufariki dunia baada ya kufanya mtihani wa Biolojia mnamo Ijumaa iliyopita.

Kulingana na mkurugenzi wa elimu wa Rarieda, Elijah Adie, mtahiniwa huyo alikuwa amesema alikuwa na maumivu ya kifua.

Mkurugenzi wa elimu alisema mwalimu alimkimbiza mtahiniwa huyo katika hospitali ya Lwak ambako aliaga dunia alipokuwa akiendelea kutibiwa.

“Mvulana huyo alikuwa mgonjwa lakini alionekana thabiti kulingana na mkuu wa shule hiyo Bi Eunice Juma,” akasema Bw Adie.

You can share this post!

Changamoto ya kuwa mcheshi ungali chuoni

Ruto amtafute Mzee Moi amsamehe – Atwoli

adminleo