Habari za Kitaifa

Mwanafunzi apatikana amefariki kwa kinachodaiwa ni kujitia kitanzi kwa kukosa karo

January 17th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

WINGU la simanzi limegubika kijiji cha Mogoroka katika eneobunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira baada ya mwanafunzi wa Kidato cha Pili kupatikana akiwa ameaga dunia kwa kinachodaiwa ni kujinyonga kwa kukosa karo.

Mwanafunzi huyo Josphat Mayaka,15, anasemekana kujitia kitanzi usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii ndani ya nyumba yake.

Kulingana na wazazi wake, hali yao ya uchochole ndiyo ilikuwa imewafanya wachelewe kumlipia karo ya Sh20,000.

Lakini wazazi hao–Bw Philip Mayaka na Joyce Nyanchera–walikuwa wamemsihi kijana awe na subira wakitafuta pesa hizo ili wamlipie pamoja na dada yake mwingine anayemfuata. Dada yake anafaa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

“Sisi ni watu wa mapato ya chini sana na tunaishi maisha ya kubahatisha jinsi mwonavyo. Lakini tulikuwa tumemhakikishia kuwa tungemlipia karo hiyo, bora tu awe na subira,” mzee Philip Mayaka amesema wakati Taifa Leo imefika nyumbani kwake.

Mzee huyo alieleza kuwa walishangaa ni kwa nini mwana wao hakuwa ameamka kama siku nyingine na hivyo wakaamua kuenda kumwamsha.

“Redio ilikuwa inasikika kutoka kwa nyumba yake hadi saa tano asubuhi. Tulishangazwa na hilo kwani si kawaida yake. Ilitulazimu tuende kubaini kilichokuwa kikiendelea. Mlango na dirisha vilikuwa vimekomelewa kutoka ndani. Tulivunja dirisha na kuingia ndani na tukakuta akiwa ananing’inia kutoka darini huku akiwa amejifunga neti ya kuzuia mbu,” mzee Mayaka akaongeza.

Mama ya mwendazake alilemewa na hisia na alilia kwa uchungu mwingi kutokana na kifo cha mwanawe.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Hema.

Mzee Mayaka alisema namna walivyokuwa wamepanga.

“Marehemu alikuwa akisomea katika Shule ya Upili ya Bobaracho. Tulikuwa tumepanga kama tungepata karo hiyo, tumlipie nusu na dada yake mwingine aliyefanya KCPE 2023 alipiwe nusu nyingine,” mzee huyo aliongeza.

Bw Mayaka alitoa ombi kwa Wakenya wenye nia nzuri wamsaidie bintiye huyo, ambaye hajajiunga na Kidato cha Kwanza kufanikisha ndoto yake.