Habari Mseto

Mwanafunzi ashtakiwa kuiba Sh600,000

April 17th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi Christol Noel Warriah alishtakiwa Jumatano kwa kosa la kuiba Sh600,000.

Warriah alikanusha mashtaka ya wizi kutoka kwa gari lililokuwa limefungwa na kuegeshwa.

Mahakama ilielezwa mshtakiwa alitekeleza uhalifu huo Februari 29.

Alishtakiwa aliiba kutoka gari la Antony Gitari Muriithi.

Mshtakiwa aliyewakilishwa na wakili Wambugu Wanjohi aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka James Gachoka hakupinga ombi hilo.

Hakimu mwandamizi Martha Nanzushi aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh100,000 na kuamuru kesi itajwe April 30, 2020.