Habari Mseto

Mwanafunzi ashtuka kuambiwa adhabu ya kuiba simu ni kifo

May 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa shule ya upili mwenye umri wa miaka 18 alishtakiwa Jumanne kwa wizi wa mabavu ambao adhabu yake ni kifo akipatikana na hatia ama kifungo cha maisha gerezani.

Punde tu alipofahamishwa adhabu ya kesi inayomsubiri alishtuka na kuomba mahakama imsaidie.

Grophat Wanjala Muruli (pichani) aliyemsihi hakimu amsaidie kusaka wakili wa kumtetea kwa vile adhabu inayomkondolea macho ni kali alisema “sikujua nitafunguliwa mashtaka makali jinsi hii. Ikiwa nitanyongwa basi nahitaji kusaidiwa.”

Awali hakimu mkuu Francis Andayi alimwuliza mwanafunzi huyo “mbona unajiingiza kwa uhalifu wa kiwango cha juu jinsi hii. Unajua kwamba adhabu ya mashtaka yanayokubali ni kunyongwa ama kutumikia kifungo cha maisha?”

“Hebu nikuulize ni kitu gani kiliendelea kabla ya wewe kushikwa,” Bw Andari alimwuliza mshtakiwa.

“Nilikuwa naendesha kibao chenye magurudumu nilipovamiwa na washambulizi walionipiga na kuninyang’anya simu pamoja na ile nilikuwa nimechukua,” alijibu Wanjala.

“Mbona walikupiga? Ulipigwa kwa sababu ulimnyang’anya kwa nguvu Josiah Mwangi Wango simu yenye thamani ya Sh18,000. Kumbe wakati mnafanya skating na wenzako huwa mnachunguza mtakaowapora.

Basi siku zako 40 amhazo mwizi huiba kabla ya kukamatwa zilitimia ulipokamatwa,” alisema Andayi akiongeza , “Si huu ni ule ujinga tu vijana mnajiingiza katika uhalifu pasi kufungua macho?”

Hata hivyo Bw Andayi alimweleza bodi ya masuala ya sheria la mahakama itamsaidia kupata wakili wa kumtetea kwa “vile adhabu yake ni kifo akipatikana na hatia.”

Hata hivyo mshtakiwa alikubaliwa kuwasilisha ombi la dhamana baada ya afisa wa urekebishaji tabia kumhoji yeye pamoja na familia yao.

Kesi itatajwa Mei 23. Alikana  alimnyang’anya kimabavu Bw Wangu simu ya rununu mnamo Mei 13, 2018. Itasikizwa Julai 3, 2017.