Habari Mseto

Mwanafunzi atoweka shuleni mara baada ya umeme kupotea

October 21st, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

POLISI Kaunti ya Lamu wanamtafuta mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyeripotiwa kutoweka kwenye shule ya upili ya wasichana ya Lamu tangu Jumamosi usiku.

Mwanafunzi huyo inadaiwa alitoroka shuleni mwao bila ruhusa pindi umeme ulikatika Jumamosi.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bi Jamila Mohamed amedinda kuzungumzia suala hilo akidai hakuwa shuleni wakati msichana huyo alitoweka.

Badala yake, Bi Mohamed ameelekeza wanahabari kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Elimu, Kaunti ya Lamu, Bw Joshua Kaaga, akisema yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kuzungumza kwa vyombo vya habari kuhusu masuala ya elimu Lamu.

Katika mahojiano na wanahabari ofisini mwake Jumatatu, Bw Kaaga amethibitisha kupotea kwa msichana huyo na kufichua kuwa inaaminika huenda amejificha nyumbani kwa mpenzi wake.

“Ni kweli. Kuna msichana aliyetoroka shuleni Lamu Girls tangu Jumamosi. Hakupewa ruhusa na utawala wa shule. Uchunguzi wetu unatuelekeza kwa fununu kuwa yuko katika uhusiano ya kimapenzi mjini na huenda amejificha nyumbani kwa mpenzi wake. Tumepiga ripoti kwa polisi na uchunguzi zaidi unaendelea kubainisha mahali halisi ambako mwanafunzi huyo amejificha,” amesema Bw Kaaga.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, amethibitisha kuwa ripoti tayari imepigwa katika kituo cha polisi cha Lamu na kwamba msako umeanzishwa wa kubainisha alipo msichana huyo ili arudishwe shuleni.

“Walimu walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Lamu leo (Jumatatu) asubuhi. Inasemekana msichana alitoroka shuleni usiku wa kuamkia Jumamosi na kuhamia kwa mpenzi wake mtaa wa Kashmir, lokesheni ya Langoni mjini Lamu. Polisi tayari wanaendeleza msako wa kubainisha mahali halisi aliko mwanafunzi huyo,” amesema Bw Macharia.

Baba wa mwanafunzi huyo, ameelezea kushtushwa kwake na kutoweka kwa bintiye shuleni.

Mzazi huyo amesema hakuna hata siku moja ambapo ameitwa shuleni kuhusu utovu wa nidhamu unaomhusisha bintiye.

“Huyo ni msichana wangu wa kwanza. Nina watoto wanne. Yeye pekee ndiye yuko sekondari. Wengine wote wako shule ya msingi. Wasiwasi wangu ni kwamba sielewi hali ya msichana wangu popote alipo kwa sasa. Polisi, utawala wa shule na hata umma unisaidie kujua aliko binti yangu. Ni tegemeo kubwa kwa familia yetu,” amesema mzazi huyo wa kiume.

Naye mamake mwanafunzi huyo amesema kamwe hajachoka kumwadilisha na kumpa mawaidha bintiye kila mara anapoondoka nyumbani kuelekea shuleni; hasa kila wakati shule zinapofunguliwa.

“Nimekuwa nikimuonya kuepuka marafiki wabaya na utovu wa nidhamu. Ninashangaa kwamba ametoweka shuleni na wala hatujamuona nyumbani. Ni siku ya tatu sasa. Ninaomba wanaomfahamu aliko wapige ripoti kwa polisi mara moja,” amesema mama ya msichana huyo.