Dondoo

Mwanafunzi fisi akosa ufadhili kwa kubainika anapenda sketi sana

January 2nd, 2024 1 min read

KAPCHERANY, SOTIK

Na NICHOLAS CHERUIYOT

JAMAA wa hapa aliamua kuacha kumsaidia kakake alipogundua kwamba polo ni sponsa wa kipusa mmoja licha ya kuwa na mke na watoto.

Mdaku wa makala anaarifu kuwa kaka mdogo wa jamaa alimlilia amlipie karo ya chuo kikuu naye akaamua kumsaidia kwani ana uwezo wa kutosha.

“Jamaa aliamua kwenda chuoni licha ya umri wake mkubwa. Kaka alivutiwa na ari yake na akaamua kumpiga jeki,” akaarifu.

Juzi, jamaa alishangaa kuwa nduguye anagharimika vilivyo kwa mpango wa kando na akaamua kukatiza usaidizi kwake.

“Kwa sasa wazee wa boma wanajaribu kumtuliza jamaa amsamehe kakake ambaye ameahidi kumtema kimada wake mara moja,” akasema msimulizi.

***

Janadume nafiki lenye mazoea ya ‘kugeuza kibao’ lapatikana peupe

LIKONI, MOMBASA

Na JANET KAVUNGA

MWANADADA wa hapa alipandwa na hasira baada ya kugundua kuwa mumewe aliyemlaumu kwa kuchepuka alikuwa na vimada kadhaa.

Demu alisema kuwa lengo la mumewe kumsingizia uasherati lilikuwa ni kuficha tabia yake ya uzinifu.

Ni dada ya demu aliyempata jamaa kwa demu mmoja na alipochunguza akaelezwa na majirani kuwa wanamfahamu kama mume wa jirani yao.

“Alipomweleza dada yake, alifunguka macho na kuanza uchunguzi wake na akabaini mumewe alikuwa akichepuka na wanawake kadhaa.

“Alikasirika na kumkabili akitisha kumuacha iwapo ataendelea na tabia hiyo. Jamaa alikubali kwamba alikuwa na mipango ya kando na akaahidi kubadilisha tabia,” alisema mdokezi