HabariSiasa

Mwanafunzi mjanja wa Moi

November 7th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amejitokeza kuwa kiongozi mjanja wa siasa sawa na alivyokuwa mlezi wake wa kisiasa, Rais mstaafu Daniel Moi hasa katika kumaliza nguvu taasisi kuu za kuendeleza demokrasia.

Ingawa anatawala katika mazingira tofauti na Mzee Moi aliyehudumu chini ya katiba iliyompa nguvu na mamlaka makuu, Rais Kenyatta amekuwa akitumia mbinu zinazofanana na alizotumia rais huyo wa pili wa Kenya kuzima upinzani na wanaokosoa serikali yake.

Wadadisi wanasema kwa sababu ya mipaka aliyowekewa na katiba ya sasa, Rais Kenyatta anatumia ujanja wa kisiasa kusukuma ajenda za serikali hata kama zinapingwa na Wakenya wengi, hatua ambayo imezorotesha demokrasia.

VYAMA VYA UPINZANI NA BUNGE

Hatua ya kwanza ya Rais Kenyatta katika kipindi chake cha pili cha utawala ilikuwa ni kumaliza upinzani dhidi ya serikali yake, sawa na alivyofanya Mzee Moi mnamo 1982 alipobadilisha katiba na kuweka kifungu cha 2A kufanya Kenya nchi ya chama kimoja.

Kutokana na vikwazo vya kikatiba, Rais Kenyatta alitumia mbinu iliyojaa ujanja. Kwanza aliunganisha vyama vya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 ili kuunda chama cha Jubilee Party.

Hatua hii ilikuwa sawa na ile Mzee Moi aliyotumia 1997 wakati alipomrai Raila Odinga kuunganisha chama chake cha National Development Party (NDP) na Kanu ili kubuni New Kanu.

Msumari wa mwisho uliolemaza upinzani ulikuwa ni handisheki na Bw Odinga, jambo ambalo lilizima sauti za wakosoaji ndani na nje ya bunge.

Hatua hii imempa Rais Kenyatta uhuru wa kupitisha kila anachotaka bungeni bila pingamizi zozote kwani waliokuwa wapinzani hasa katika ODM sasa wanacheza ngoma ya Jubilee.

VYOMBO VYA HABARI

Chini ya utawala wake, Mzee Moi hakuruhusu uhuru wa habari kunawiri inavyohitajika katika demokrasia.

Alihakikisha Wakenya walitegemea shirika la KBC pekee kupata habari, kuwanyima leseni watangazaji huru, kupiga marufuku majarida yaliyokosoa utawala wake pamoja na wanahabari kutishwa, kukamatwa na kutupwa kizuizini kwa madai ya uhaini.

Rais Kenyatta kwa upande wake amekuwa akilaumu vyombo vya habari kila vinapofichua kashfa ama kukosoa serikali yake, pamoja na kudhalilisha magazeti machoni pa umma hasa anaposema ni “ya kufunga nyama”.

Wanablogu wa serikali nao wamekuwa wakiwashambulia baadhi ya wanahabari ama mashirika ya habari yanayojaribu kukosoa utawala wa Jubilee.

Serikali pia imelemaza vyombo vya habari kifedha kwa kupunguza matangazo.

MASHIRIKA YA KIJAMII

Serikali imekuwa ikizima mashirika ya kijamii kupitia vitisho na kuyawekea vikwazo vya kisheria.

Baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakikamatwa wakijaribu kuandamana kulalamikia au kupinga sera na maamuzi ya serikali licha ya kuwa maandamano ni haki ya kikatiba.

Vikwazo vya kisheria navyo vimehakikisha mashirika hayo hayawezi kupata misaada ya kifedha kutoka nje ya nchi ili yasiwe na nguvu za kukosoa serikali na bodi ya kuthibiti mashirika hayo imekuwa ikifunga yanayokosoa serikali ikidai yamekiuka sheria.

Hatua hizi ni sawa na mbinu za serikali ya Mzee Moi ambaye alitumia kila njia kuyanyamazisha. Katika miaka 24 ya utawala wake, mashirika yasiyo ya serikali hasa yaliyohudumu maeneo ya upinzani yalikuwa yakifungwa, wanaharakati kukamatwa na kutishwa hadharani.

KUZIMA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

Moi hakutaka vyama vya wafanyakazi vilivyokuwa na nguvu au vilivyoweza kusababisha uasi dhidi ya serikali yake. Alipiga marufuku chama cha kutetea maslahi ya watumishi wa umma, muungano wa wenye matatu na kile cha wahadhiri wa vyuo vikuu na kuwakamata baadhi ya viongozi wake wakiwemo aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga na Katama Mkangi.

Rais Kenyatta kwa upande wake anaonekana kutumia mbinu sawa na za mlezi wake kisiasa katika masaibu yanayoandama chama cha Knut, ambacho kimekuwa mwiba kwa serikali yako kinapotetea walimu.

Jubilee imetumia ujanja kuvuruga uongozi wa chama hicho. Baada ya kushindwa kuondoa Katibu Mkuu William Sossion kwa kupinga sera za elimu za serikali hasa mtaala mpya, Tume ya Uajiri wa Walimu (TSC) imemwondoa kwenye orodha ya walimu na sasa inataka kukivunjilia mbali Knut.

MAHAKAMA

Sio siri kwamba Rais Uhuru Kenyatta hafurahishwi na utendakazi wa mahakama ambayo chini ya katiba ya sasa imehakikishiwa uhuru wake.

Amefanya juhudi za wazi kupunguza uhuru huo kwa kukataa maazimio ya Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC), kuinyima pesa, kutisha hadharani na kulaumu majaji kwa madai ya kutotekeleza majukumu yao.

Rais Kenyatta anajaribu kuiga Mzee Moi ambaye alitawala chini ya katiba iliyompa mamlaka ya kuteua majaji ambao angeweza kushawishi.