Kimataifa

Mwanafunzi wa chekechea ashtua shule kufika akiwa na bunduki

January 14th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MTOTO wa miaka sita nchini Marekani alishangaza watu wakati alipofika katika shule ya chekechea anaposomea akiwa amebeba bunduki Ijumaa.

Iliripotiwa kuwa mtoto huyo kutoka jimbo la Ohio alionekana kuwa na kitu kizito kwenye suruali yake alipofika katika shule hiyo ya Columbus Africentric Early College, ndipo akapatikana kuwa na bunduki, japo polisi hawakuripoti ikiwa ilikuwa na risasi.

Hata hivyo, picha walizosambaza polisi zilionyesha bunduki pamoja na risasi zilizoaminika kupatikana pamoja na bunduki hiyo.

“Wafanyakazi wa shule walishauriwa na mtu aliyewapigia simu kuwa  mwanafunzi huyo alikuwa akiingia shuleni na kitu kilichoonekana kuwa kizito katika suruali yake,” polisi wakasema.

“Mwanafunzi huyo alikabiliwa mlangoni na bunduki ya mkononi ikapatikana.”

Hata hivyo, polisi walisema kuwa hawatamfungulia mashtaka mtoto huyo kwani nimchanga sana. Lakini wanachunguza mahali alitoa silaha hiyo.

Shirika moja la habari nchi hiyo liliripoti kuwa kupitia barua, mwalimu mkuu wa shule hiyo alisema kuwa mwanafunzi huyo “ataadhibiwa ifaavyo” japo bila maelezo zaidi.

Ripoti hiyo ilisema mwalimu huyo, Tyree Pollard alisisitiza namna shule hiyo hairuhusu silaha, huku akirai wazazi kushauri wanao kutofika na vitu hivyo shuleni.

“Watu wachanga wanafaa kufahamu hatari za kuwa na bunduki ama silaha nyingine, hata ziwe feki zinazokaa kuwa za kweli,” Pollard akaandika.

Alisema kuwa familia zinafaa kuzungumza na wanao kuhusu vitu ambavyo havifai kamwe kufikishwa shuleni.