Habari Mseto

Mwanafunzi wa JKUAT motoni kwa kulaghai mhadhiri Sh1.4m

May 22nd, 2018 1 min read

Mshukiwa Emmanuel Okwach na wakili wake Davud Ayuo (kushoto) akiwa kortini Jumatatu kwa kupokea Sh1.4milioni kwa njia ya udanganyifu. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa chuo kikuu Jumatatu alishtakiwa kupokea Sh1.4 milioni kutoka kwa mhadhiri akimdanganya zilikuwa za kugharamia matibabu ya nduguye.

Emmanuel Okwach , ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha JKUAT alikana alimlaghai Bi Joyce Cherono Sh1.4milioni akidai zilikuwa za kumpeleka nduguye Kelvin Habib hospitali.

Mshtakiwa alikana alipokea kitita hicho cha katika muda wa miezi mitano kati ya Januarin 1 na Mei 18 mwaka huu.

Wakili David Ayuo anayemwakilisha mshtakiwa alimwambia hakimu mkuu Bw Francis Andayi “mshtakiwa anatoka jamii maskini na kwamba hawezi kupata dhamana ya kiwango cha juu.”

Bw Ayuo alimsihi hakuwa “atilie maanani hali ya uchochole ya mshtakiwa akimwachilia kwa dhanana.”:

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh100,000.

Ikiwa mshtakiwa hatafanikiwa kupata dhamana hiyo ya Sh100,000, hakimu Andayi aliamuru ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia amhoji pamoja na watu wa familia yake wabaini ikiwa anatoka jamii maskini.