Habari Mseto

Mwanafunzi wa Kidato cha Nne afariki kwa corona

November 17th, 2020 2 min read

BENSON AMADALA na DERICK LUVEGA

MWANAFUNZI wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Elizabeth Lureko eneo la Mumias Magharibi amefariki baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Mwanafunzi huyo alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Lifecare, Bungoma. Anashukiwa kuambukizwa gonjwa hilo aliposafiri nyumbani kwao na kutangamana na wazazi wake ambao pia walipatikana na virusi hivyo.

Kifo cha mwanafunzi huyo kimejiri wakati shule katika eneo la Magharibi zimeripoti kuongezeka pakubwa kwa maambukizi miongoni mwa wanafunzi wanaojiandaa kwa mtihani wa Kitaifa wa Sekondari (KCSE) mwaka ujao.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Kakamega, Dkt Collins Matemba alisema wazazi wa msichana huyo walikuwa wameambukizwa na kwa sasa wanapokea matibabu nyumbani kwao eneo la Mumias Magharibi.

Mwanafunzi huyo aliripotiwa kusafiri nyumbani kabla ya hali yake kuzorota ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya St Mary Mumias na kisha kuhamishiwa Hospitali ya Lifecare baada ya hali yake kuzorota.

“Tumetuma vikosi vya afya ya umma shuleni humo kuangazia hali na kuweka mikakati ya kusaidia kukabiliana na kuongezeka kwa maambukizi,” alisema Dkt Matemba.

Katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Sacred Heart Mukumu, mwanafunzi wa Kidato cha Nne aliyeanza kuugua, alithibitishwa baadaye kuambukizwa Covid-19 lakini akatoroka hospitalini alikolazwa.

Mwanafunzi huyo alilazwa katika Hospitali ya Misheni ya St Elizabeth lakini akaripotiwa kutoweka kutoka wadi na hajulikani alipo kwa sasa.

Ilidaiwa alitoroka na mvulana anayeaminika kuwa mpenzi wake.

Hayo yamejiri huku Kenya ikiandikisha visa 599 zaidi vya Covid-19 na kufanya jumla ya maambukizi nchini kufikia 70,804 katika muda wa saa 24. Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Waziri Mutahi Kagwe alitangaza kuwa visa hivyo vipya vinajumuisha Wakenya 541 na raia wa kigeni 18 ambao miongoni mwao 336 ni wanaume na 223 wanawake.

Wakati huo vilevile, wagonjwa 478 walipona kutokana na gonjwa hilo wakiwemo 337 waliokuwa wakihudumiwa nyumbani na 141 kutoka hospitali mbalimbali kote nchini, na kufanya jumla ya waliopona kufikia 46,244.

Hata hivyo, idadi ya vifo imefikia 1,287 baada ya wagonjwa 18 zaidi kufariki.

Kulingana na Waziri, chembechembe 3,074 zilifanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 na kufanya jumla ya watu waliopimwa kufikia sasa kuwa 793,026.