Makala

Mwanafunzi wa sekondari awafaa wenzake wa shule za msingi Kiandutu

June 12th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI popote walipo wanastahili kuendelea kujisomea wenyewe nyumbani huku wakingoja kurudi shuleni mambo yakirejea kawaida.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Rongai Boys High Bw Amos Ngure amejitokeza kuwa mwokozi wa wanafunzi kijijini.

Ngure amesema yeye kama mkazi wa kijiji cha Kiandutu mjini Thika, amejitolea kuwapa mafunzo ya bure wanafunzi wa shule za msingi ili wazidi kujiimarisha masomoni.

“Wanafunzi wengi walio vijijini hawana uwezo wa kupata simu za kidijitali ili kusomea nyumbani; na kwa hivyo inabidi wafundishwe kwa njia ya kawaida,” anasema Ngure.

Anasema aliwaza na kupata ya kwamba wanafunzi wengi wanakosa kazi ya kufanya huku wakionekana wakicheza mitaani.

“Mimi kama mwanafunzi aliye na ari ya masomo nilifanya juhudi kuwaleta pamoja ili niwape mwongozo jinsi wanavyoweza kujikumbusha walichokisoma shuleni,” anasema.

Anasema hata ingawa shule zinatarajia kufunguliwa mwezi Septemba, ni vyema wanafunzi kujitayarisha kwa masomo badala ya kuketi bure.

Anamshukuru Dkt Susan Gitau kwa kumkuza ili kufika kiwango hicho alichofikia.

“Dkt Gitau amekuwa kielelezo kwa wakazi wa Kiandutu kwa kuwasaidia na chakula na mawaidha kimawazo,” anasema Ngure.

Kwenye mahojiano ya runinga ya hapa nchini mnamo Alhamisi, Dkt Gitau alisema wakati huu wa janga la Covid-19, Wakenya wengi wamekuwa na wasiwasi mwingi kuhusu hali yao ya baadaye.

Dkt Gitau ambaye ni mwanasaikolojia na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nazarene, alisema wakati huu wa Covid-19 familia nyingi haziko pamoja kimawazo.

“Wakati huu unapata watoto wakilia zaidi, na watu wazima wakiwa na hasira tele; jambo ambalo linatokana na kutatizika kimawazo,” alisema Dkt Gitau.

Anasema kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, hii corona itasababisha watu 50 milioni kukumbwa na makali ya njaa.

Alisema kwa miezi mitatu ambayo imepita hali ya maisha imebadilika kwa wengi kwa sababu biashara tayari zimezorota, huku viwanda vingi vikifungwa na watu kupoteza ajira zao.

Hata hivyo, alitoa mwito kwa watu kutopoteza matumaini kwa sababu kila kitu kina muda wake.

Alisema wakati kama huu ni wa kuvumiliana na kuwa na upendo licha ya mambo kuwa magumu.

“Tabia ya binadamu kwa kawaida unakabiliwa na shida unakuwa na wasiwasi, lakini ni vyema kujizuia ili kupunguza hasira za kila mara,” alisema Dkt Gitau.