Habari Mseto

Mwanafunzi wa UoN kizimbani kwa kuchoma jengo

March 22nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa Chuo kikuu cha Nairobi (UoN) alishtakiwa Alhamisi kwa kuchoma jengo lenye thamani ya Sh14,493,027 miaka miwili iliyopita.

David Ochieng Osano , aliye katika mwaka wa nne katika chuo hicho alikanusha shtaka dhidi yake alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi , mahakama ya milimani Nairobi Bw Peter Ooko.

Osano alimweleza hakimu alikuwa ameachiliwa kwa kosa hilo lakini akatiwa nguvuni tena na kufunguliwa mashtaka katika kituo cha polisi cha Kilimani.

“Kesi dhidi yangu ilikuwa imetamatishwa kisha nikashikwa tena kwa makosa yayo hayo,” alisema Osano.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

“Nilikuwa nimeachiliwa kwa dhamana ya Sh80,000 pesa tasilimu,” alisema Osano.

Osano alikabiliwa na shtaka la kuchoma jengo la Students Welfare Authority (SWA) mnamo Oktoba 2 2017.

Thamani ya jengo hilo ni Sh14,493,027. Adaiwa alikuwa anashirikiana na wanafunzi wengine ambao wameshtakiwa tayari. Kesi itaunganishwa.