Habari

Mwanahabari abubujikwa na machozi baada ya kuponea kusukumwa ndani

May 10th, 2018 2 min read

Na RICJARD MUNGUTI

MWANAHABARI alidodokwa na machozi Jumatano kortini baada ya polisi kunyimwa fursa ya kumzuilia siku saba kuhusiana na shambulizi la mfanyabiashara katika hoteli moja jijini Nairobi.

Bw Sangira Stephen Ochola, ambaye picha yake ilisambazwa mitandaoni kutokana na shambulizi la Bw Timothy Muriuki mnamo Aprili 30, 2018 alishindwa kujimudu na kujipata akitiririkwa n amachozi baada ya hakimu mkazi Bi Miriam Mugure kusema “hakuna ushahidi wowote uliomhusisha mwanahabari huyu na kisa cha kutwangwa kwa mlalamishi.”

Bw Stephen Sangira kabla ya kesi dhidi yake kuanza hapo Mei 9, 2017 katika mahakama ya Milimani, Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Mahakama iliambiwa hakuna utambuzi mwingine unahitajika kwa vile picha ya Ochola imeonekana kote ulimwenguni baada ya kuchapishwa na magazeti  ya Taifa Leo na Daily Nation.

Mawakili  Cliff Ombeta, Nelson Havi , Michael Osundwa , Rodger Sagana  na Harun Ndubi walimweleza hakimu polisi wanataka kumtesa mshukiwa.

Akimhoji afisa anayechunguza kesi hiyo  Koplo Francis Mwita , Bw Ombeta alimtaka aeleze ikiwa Bw Ochola alitiwa nguvuni wakati mmoja na Mbunge wa zamani wa Kamkunji Simon Mbugua  na mabroka  Antony Otieno Ombok almaarufu Jamal  na Benjamin Odhiambo Onyango almaarufu Odhis mnamo Mei 8, 2018.

Mwanahabari apandwa na hisia baada ya kuona jinsi mawakili walimenyana katika kesi dhidi yake. Picha/ Richard Munguti

Koplo Mwita alikiri aliwatia nguvuni wote wanne wakati mmoja.

“Mbona hukumfungulia mshtaka ya wizi wa mabavu wakati mmoja na Mabw Mbugua, Ombok na Onyango?” Bw Ombeta akauliza.

“Sikuwa nimekamilisha uchunguzi kwa vile kuna washukiwa wengine wanaoendelea kuswakwa na polisi,” alijbu Koplo Mwita.

Koplo Mwita aliomba korti iamuru mshukiwa huyo azuiliwe kwa siku saba ndipo “walalamishi wajitokeze kumtambua kwa vile anashukiwa amehusika katika visa vingine vingi vya kuwashambulia watu.”

Machozi yaanza kumdondoka mwanahabari alipoona dalili kuwa hatasukumwa ndani siku saba. Picha/ Richard Munguti

Mahakama iliambiwa Koplo Mwita anamtesa mshukiwa huyo.

“Kubali tu unamtesa mshukiwa huyu,” Bw Ombeta alimwambia polisi huyo.

“Hapana,” alijibu Koplo Mwita.

Mawakili Ndubi , Sagana na Havi walisema kile mahakama inaweza kufanya ni kumwachilia mshtakiwa kwa dhamana kwa vile “tayari afisa mkuu wa polisi Ireri Kamande ameshasema hawatamshtaki  Bw Ochola.”

Jaji alipotaja kuwa Bw Sangira aachiliwe kwa dhamana ya Sh100,000, hakuweza kuvumilia, aliyaachilia machozi yakambubujika. Picha/ Richard Munguti.

Bi Mugure alitupilia mbali ombi la kumtaka Bw Ochola azuiliwe kwa siku saba.

Pia alisema Koplo Mwita hakuwa ameitia saini ombi alilowasilisha kortini akiunga mkono kuzuiliwa kwa mshukiwa huyo.

Korti ilimwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa tasilimu kisha ikamwamuru afike mbele ya koplo Mwita kuhojiwa.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Mei 14, 2018.