Makala

Mwanahabari aliyepuuza wito wa kujitoma kwa siasa akasalia mhisani wa jamii

May 4th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

JOHN Rapudo kutoka Kijiji cha Eshikarame, Wadi ya Musanda, Kaunti ya Kakamega anafadhili masomo ya wanafunzi wa shule za kutwa kwa kuwalipa karo na hata chakula.

Bw Rapudo alisomea taaluma ya uanahabari katika chuo kikuu cha Multimedia, na amejitolea kusaidia jamii yake kutokana na umaskini unaowaandama.

Alisema wazazi wengi kwenye wadi hiyo wanakabiliwa na umasikini ambao hauwaruhusu kulipa karo ya shule jinsi inavyofaa.

“Huwa haifurahishi. Natembea vijijini nakutana na wanafunzi ambao hawajaenda shulen Kile kidogo napata na familia yangu najitolea kulipa karo yao,” alisema Bw Rapudo.

Huku shule zikitarajiwa kufunguliwa wakati wowote na Serikali kwa Muhula wa Pili, alisema amekuwa akipata vilio vya wazazi kupitia jumbe au kuonana ana kwa ana wakihitaji usaidizi.

“Katika muhula huu wa pili, ni wanafunzi 150 ambao wamepokea hundi za basari. Kila mmoja amepata usaidizi kulingana na karo iliyosalia shuleni. Kuna wale wamepokea Sh5,000, Sh3,000, Sh2,000 na wengine Sh1,500,” aliongeza Bw Rapudo, 32.

Aliambia Taifa Leo Dijitali alikuwa yatima akiwa shule ya upili na matatizo aliyopitia kwa kipindi cha miaka mitatu, yalifanya akawa na msukumo wa kutoa.

“Sio wanafunzi pekee ninaosaidia. Kuna wale wajane ambao hawana nyumba. Najikakamua kuhakikisha wanapata nyumba. Hapo kwa ujenzi natafuta msaada kwa marafiki ambao wanaelewa matatizo,” alieleza Bw Rapundo.

“Pia, kuna wale ajuza hapa kwetu hawana malazi. Hawajawahi kutumia kitanda wengi hutumia jamvi,” aliongeza.

Hata hivyo, mwanahabari huyo amemsifia mkewe ambaye pia humpiga jeki kwa kununua magodoro anapohitaji.

“Nafikiri kile unachoomba Mungu hukupa. Mke wangu pia ana utu na moyo wa kutoa. Kutokana na biashara yake, wakati mwingine hununua godoro za ajuza na kunipa nipeleke,” alisifia Bw Rapudo.

Aliambia Taifa Leo licha ya kushinikizwa kuingia kwenye siasa, atasalia kufanya kazi ya uanahabari.