Habari

Mwanahabari asimulia mateso mikononi mwa polisi bandia

February 6th, 2019 3 min read

Na WYCLIFFE MUIA

MWANAHABARI Wambui Wakobi wa kituo cha televisheni cha Kameme aliteseka mikoni mwa watu aliodhani kuwa maafisa wa polisi hapo Januari 30, 2019.

Bi Wakobi alikuwa anaendesha gari lake kutoka Hospitali ya Kijabe na baada ya kufika eneo la Kiracha karibu na msitu wa Kamae, alisimamishwa na watu wawili waliovalia na sare za polisi.

Maafisa hao bandia wa polisi walikuwa wameandamana na jamaa mmoja ambaye hakuwa na sare za polisi aliyevalia t-shati nyekundu.

Madam, kwa nini unaendesha gari kwa kasi?” wakamuuliza. Wambui akajibu, “Mimi siendeshi gari mbio kwa sababu hata hii barabara imejaa mashimo.”

Majambazi hao walimuitisha leseni yake ya kuendesha gari ambayo alikuwa ameiweka ndani ya mfuko uliokuwa nyuma ya gari.

“Kabla nifungue mfuko nichukue leseni, mwanamume mmoja alichukua ufunguo wa gari langu na kuniamrisha nitoke nje. Alinimbia nimekamatwa na polisi.”

Aliwauliza mara kadhaa kwa nini amekamatwa, bila kupewa jibu, na punde wakampeleka katika gari lingine lililokuwa upande mwingine wa barabara.

“Hapo ndipo niling’amua kuwa hao si polisi, ni majambazi,” akasimulia.

Walimkalisha nyumba ya gari, katikati yao na kumwamrisha apeane simu na aeleze mahali ufunguo fiche wa gari almaarufu ‘cut-off’ kilipo.

Walifunga milango ya gari na kumtaka ajitambulishe huku wakianza safari kuelekea eneo ambalo hakujua.

Madam unaitwa nani?” wakamuuliza. “Naitwa Wambui,” alijibu.

Mahojiano kwa Kikuyu

Baada ya kutaja jina, walibadilisha lugha mara moja wakaanza kumhoji kwa Kikuyu.

“Rîu Wambui rî, ithuî tûtirî borithi. Ithûî túrî mîici na wîra wiitû nî kûiya na kûraga.” (“Sasa Wambui, sisi si polisi. Sisi ni wezi na kazi yetu ni kuiba na kuua”).

“Mwili wangu uliganda na nikaanza kulia,” anasema.

Majambazi hao walimuonya iwapo hatatulia na akatae kutii amri zao, basi angekiona cha mtema kuni.

“Jambazi aliyekuwa mkono wangu wa kulia alinipatia kitambaa nikajipanguza machozi na nikajifanya kutulia.”

Kufikia sasa, gari walimokuwa lilikuwa linaelekea katika msitu wa Kamae na kabla ya kufahamu mahali walipokuwa wanaenda walimfunika macho.

“Niliwasihi wasinifunge mapua na wakapandisha kitambaa eneo la macho pekee huku wakiniahidi kuwa hawawezi niua hadi watimize njama yao.”

Wizi wa hela kwa akaunti ya benki

Walimuitisha kadi yake ya benki pamoja na nambari ya siri, na wakamwamrisha awaelezee mahali anafanya kazi.

Aliwaelezea kuwa yeye ni mwanahabari anayehudumu Murang’a. Punde baada ya kusikia hivyo mmoja akatoa bastola na kusema, “Nyinyi wanahabari mnapenda sana kusema huwa tunabeba silaha bandia, hii ni bandia?”

Wambui ambaye alikuwa ametoka kutibiwa maumivu ya uti wa mgongo alianza kuumwa na ikabidi awaelezee masaibu yake ya kiafya.

Jambazi mmoja ambaye alionekana kuwa mkubwa wao alimtuliza lakini mwenzake hakufurahia hatua hiyo.

Wee gathee tiga kwîhe mûhiki ûyû! Úyú agútwîka gîcanjama.” (“Wewe mkubwa, acha kumpa mwanamke huyu uhuru hivyo. Atatuletea shida.”)

Mkubwa wao akamkijibu, “Achana na yeye. Anaendelea kushirikiana na sisi.”

Safari yao ilielekea mahali kulikuwa na harufu mbaya ambayo ilisababisha Wambui kutapika, hakujua ilikuwa harufu ya nini.

“Jambazi mkubwa wao aliagiza ninunuliwe maziwa na maji ili nizuie kutapika zaidi. Sikuweza kunywa maji kwa sababu ya kutapika”

Mkubwa wao alimuelezea Wambui kuwa yeye ni mhandisi ambaye hana kazi lakini wizi unamlipa vizuri sana.

“Aliniambia mkewe anaitwa Wambui kama mimi na kuwa wamewekeza sana kibiashara. Nilimahidi kumtafutia kazi baadaye lakini akakataa akionya kuwa hatupaswi kukutana tena baada ya siku hiyo.”

Safari iliendelea huku mara kwa mara wakisimama na kuenda kwa ATM wakitumia kadi yangu.

Simu ya mume

Wakiendelea na safari, mumuwe Wambui alipiga simu na wote wakanyamaza. Jambazi mkuu ambaye alikuwa na simu yake wakati huo alimuonya asifichue kinachoendelea.

“Niliambia mume wangu kuwa niko sawa na nilikuwa naelekea Murang’a alipokuwa ananisubiri. Wakati alipoendelea na maswali nilimwambia tutaongea baadaye na nikakata simu.”

Wambui alianza kuomba na baada ya kutambua kuwa alikuwa anaomba mmoja wa majambazi akamwambia kuwa awakumbuke kwa maombi lakini akamtania kuwa maombi yake hayatabadilisha mipango yao.

Baada ya mawasiliano ya muda mrefu kwa simu na jambazi aliyekuwa na gari langu, jambazi mkuu alimwambia Wambui kuwa wakati umefika wamuage.

Machozi yalimtiririka huku akiwarai wasimuue kwa sababu alikuwa akishirikiana nao bila kuwaficha chochote.

“Huwa sipeani ahadi ambazo sitatimiza. Nataka uonane na watoto wako jioni kama tu vile nitaonana na wale wangu,” jambazi mkuu alimwambia Wambui.

Gari lilisimama na akaamrishwa atoke nje na asijaribu kufungua macho.

“Jambazi mkuu alinishika mkono na tukatembea hatua chache tu. Nilimuomba anipe sekunde chache tu niseme kitu.”

Maombi

“Mungu awabariki kwa kunichunga. Naomba kila kitu mlichoniibia pamoja na gari langu viwe vya baraka kwenu.”

Jambazi huyo alisema ‘Amina’ na akamshukuru Wambui kwa kuwa mtiifu.

“Ingewezekana tungekutana tena lakini hiyo itakuwa hatari kwangu. Mungu akubariki na vitu vingi zaidi ya vile tumekuibia,” jambazi huyo alimwambia Wambui.

Walimfungua kitambaa kilichokuwa machoni na wakamuonya asiangalie nyuma.

“Nilijaribu kutembea lakini miguu yangu ilikuwa na uoga. Nilisubiri nisikie risasi nyuma yangu. Nilijipa nguvu na nikaingia ndani ya msitu bila kujua mahali nilikuwa naelekea.”

Baada ya kutembea kwa takriban dakika 40, Wambui alitokea kwenye barabara kuu na kufurahia baada ya kuona magari ya kibinafsi yakipita.

“Nilipanda matatu ambayo makanga alinieleza kuwa inaelekea Gakoe, Thika. Niliomba makanga simu niKampigia mume wangu ambaye nilimwelezea kilichotokea.”

Baadaye Wambui alikutana na mumuwe na wakaandikisha taarifa katika kituo cha Polisi cha Kijabe baada ya kupoteza gari, hela kwa benki na simu.